Hakuna mtu atakayekuwa salama hadi wote watakapokuwa salama dhidi ya COVID-19:UN 

9 Novemba 2020

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamezikosoa nchi zinazojaribu kubinafsisha na kuhodhi chanjo yoyote ya dhidi ya corona au COVID-19 inayotarajiwa kupatikana wakisema njia pekee ya kupambana na janga hili ni kuhakikisha chanjo inapatikana kwa gharama nafuu kwa kila mtu duniani.

Kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Geneva Uswisi kuhusu upatikanaji wa chanjo kwa wote wataalam hao wamesema “hakuna fursa kwa ajili ya utaifa katika vita dhidi ya janga hili. Kwani kiwango cha janga hili na gharama zake katika maisha ya watu huku kukiwa hakuna uhakika wa lini litakwisha  kinahitaji hatua zenye mrengo wa haki za binadamu na ujasiri wa kulikabili kutoka kwa nchi zote duniani.” 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa bahati mbaya kuna baadhi ya serikali zinazojaribu kupata chanjo kwa ajili ya raia wao pekee, na hii haitakuwa na manufaa kwa sababu mafanikio yoyote dhidi ya janga la COVID-19 yatategemea upatikanaji wa chanjo kwa watu wote. 

Wamesisitiza kwamba “Virusi vya COVID-19 haviheshimu mipaka, na hakuna aliyesalama hadi pale sote tutakapokuwa salama katika dunia hii iliyounganika na kutegemeana. Na nchi zinazojaribu kupata chanjo kwa ajili ya watu wake tu badala ya kushiriki kwenye juhudi za kimataifa zinazomlenga kila mtu hazitoweza kutimiza lengo walilokusudia.” 

Wataalamu hao wametoa wito kwa nchi zote kuunga mkono mkakati wa COVAX unaoongozwa na muungano wa chanjo duniani GAVI, shirikisho la kimataifa la maandalizi na ubunifu dhidi ya magonjwa ya mlipuko CEPI na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO ambao lengo lake ni kutoa fursa sawa kwa nchi zote pale chanjo ya COVID-19 itakapopatikana. 

“Chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu fursa ya chanjo yoyote ya COVID-19 lazima itapatikane kwa watu wote wanaoihitaji na katika nchi zote hususan katika maeneo yaliyohatarini zaidi au kwa wale wanaoishi katika umasikini” wamesisitiza wataalam hao. 

Pia wametoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na msaada kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kuhakikisha wanashirikiana teknolojia na njia za jinsi ya kupata chanjo na matibabu ya COVID-19 wakisema ukweli ni kwamba “Janga hili limeathiri dunia nzima na hivi sasa inapaswa kuweka kando mikakati binafsi ya kuhodhi chanjo na usambazaji wake na kufanyakazi pamoja kulitokomeza janga hili.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter