Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za haraka zahitajika kuepusha baa la njaa katika nchi nne:WFP/FAO  

Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.

Hatua za haraka zahitajika kuepusha baa la njaa katika nchi nne:WFP/FAO  

Msaada wa Kibinadamu

Mamilioni ya watu katika nchi nne zilizoghubikwa na tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula za Burkina Faso, Kaskazini mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen wanahitaji msaada wa ili kuepuka kutumbukia katika baa kubwa la njaa yameonya leo mashirika Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu. 

Akizungumza mjini Geneva Uswisi kwenye mkutano na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao Claudia Ah Poe afisa mshauri wa ngazi ya juu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP amesema “Tunatiwa hofu kwamba watu hawa wanaweza kukabiliwa na hatari kubwa ya baa la njaa endapo hali itaendelea kuzorota katika miezi ijayo.” 

Kupitia taarifa ya Pamoja na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, shirika la WFP pia limeonya kwamba nchi zingine 16 zinakabiliwa na dharura kubwa ya chakula au msururu wa dharura katika mieszi mitatu hadi sita ijayo. 

Mashirika hayo katika ripoti yao mpya kuhusu kutokuwa na uhakika katika maeneo hayo manne yamesema chachu kubwa ya migogoro hii ya kibinadamu ni Pamoja na vita vinavyoendelea na ukosefu wa fursa za kibinadamu zinazohitajika katika jamii, mabadiliko ya  tabianchi na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na janga la corona au COVID-19 

Ugawaji wa chakula na WFP kwa Watu waliohamishwa makao huko Kikuku, Kivu Kaskazini,  nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
WFP/Ben Anguandia
Ugawaji wa chakula na WFP kwa Watu waliohamishwa makao huko Kikuku, Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Mataifa yaliyo hatarini 

Ripoti ya pampja imesema mashirika yaliyo hatarini ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambako watu milioni 22 hawana uhakika wa chakula ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya watu kuwahi kuorodheshwa katika nchi moja, Ethiopia, Haiti na Venezuela. 

“Nchi hizi tayari zilikuwa na tatizo kubwa na kutokuwa na uhakika wa chakula mwaka huu wa 2020 na sasa zinakabiliwa na hatari ya hali kuzorota zaidi katika miezi ijayo.” Ameongeza Ah Poe. 

Akisisitiza kuhusu viwango vya mahitaji katika nchi tatu za Afrika zilizoko katika orodha hiyo ya nchi nne zilizo hatarini kwa baa la njaa , msemaji wa WFP Tomson Phiri ameelezea jinsi gani hali mbaya inayowakabili watu inahusiana na uasi unaoendelea Kaskazini mwa Burkina Faso na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. 

Ameongeza kuwa miaka mingi ya vita yameweka mazingira sugu ya hatihati nchini Sudan Kusini ambako mafuriko makubwa yam waka huu yamefanya hali kuwa mbaya zaidi. “Watu wamepoteza mali zao, watu wamepoteza uwezo wa kukabiliana na majanga yoyote. Tulikuwa na mafuriko mabay sana mwaka huu , maji ya mafuriko hayo yalizamisha miji, watu wanahaha, na mavuno ambayo waliyatarajia yakasambaratika.” 

Watoto wakitembea katika maji ya mafuriko katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.
© WFP/Musa Mahadi
Watoto wakitembea katika maji ya mafuriko katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

 

Athari za janga la COVID-19 

WFP na FAO wanasema takwimu za kuanzia Machi hadi Septemba zinaonyesha kuwa wakati katika nchi nyingi vikwazo kutokana na COVID-19 vinaondolewa  na kuruhusu shughuli za kiuchumi kuanza tena , hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula imekuwa mbaya zaidi katika nchi 27 na kuongeza idadi ya watu wenye kuhitaji msaada kufikia milioni 104.6. 

Mwaka 2019 idadi ya watu waliokuwa wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula katika nchi hizi 27 ilikua milioni 97.6 kwa mujibu wa WFP. 

“Katika nchi hizo 27 idadi ya watu ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula ni zaidi ya milioni 100. Tathimini bila shaka itaendelea na hivyo tunatarajia idadi hiyo kuongezeka . Na mapema mwaka huu tulikadiria katika nchi ambazo tunafanya operesheni ambazo ni takriban 80, watu wengine zaidi milioni 121 watakuwa katika hatari ya kutumbukia katika kutokuwa na uhakika wa chakula.” Amesema Ah Poe. 

Katika mji wa Dinsoor, Somalia waathirika wa kiangazi wakipokea mgao wa chakula  kutoka kwa WFP. (Maktaba)
Giles Clarke/Getty Images
Katika mji wa Dinsoor, Somalia waathirika wa kiangazi wakipokea mgao wa chakula kutoka kwa WFP. (Maktaba)

Somo walilojifunza Somalia 

Akizungumza kwa njia ya video kutoka mjini Roma Italia, afisa mchambuzi wa masuala ya mgogoro wa chakula kutoka FAO Luca Russo amekumbusha kwamba lengo kubwa la kutoa tahadhari ya leo ni kuepuka janga la kibinadamu kwa kubaini sababu nyingi zinazochangia baa la njaa nah atua gani maalum zichukuliwe kuwasaidia jamii za walio hatarini zaidi. 

Mwaka 2011 baa la njaa lilitangazwa Kusini mwa Somalia mwezi Julai lakini tayari watu wengi walikuwa wameshakufa hadi mwezi Mei. 

“Wakati unapotangaza baa la njaa tayari unakuwa umeshachelewa kuchukua hatua, kwa mantiki kwamba tumeshalishuhudia hili siku za nyuma kwa Somalia kwani wakati ambapo baa la njaa lilitangazwa tayari watu 260,000 walikuwa wameshakufa hivyo tunataka kutoa tahadhari mapema kabla baa la njaa halijatokea.” 

Akiunga mkono hilo Mkurugenzi wa masuala ya dharura na mnepo wa FAO Dominique Burgeon ametoa wito wah atua za haraka kuchukuliwa kutoka kwa kujumuiya ya kimataifa. 

“Tuna hofu kubwa kuhusu mchanganyiko wa athari za migogoro ambayo inawapora watu uwezo wa kuzalisha na kupata fursa ya chakula na kuwaacha katika hatari kubwa ya njaa iliyokithiri.Tunahitaji fursa ya kuwafikia watu hawa kuhakikisha kwamba wana chakula na njia ya kuzalisha chakula na kuboresha Maisha yao ili kuzuia janga kubwa.” Ameongeza bwana Burgeon. 

 

Mtoto anayeugua utapiamlo akipata matibabu katika hospitali Sana'a.
UNICEF
Mtoto anayeugua utapiamlo akipata matibabu katika hospitali Sana'a.

Hatari ya baa la njaa katika nchi zote 4 

Mkurugenzi wa dharura wa WFP Margot van der Velden pia ametoa tahadhari kwamba dunia iko katika hatihati ya janga kubwa kukiwa na hatari ya baa la njaa katika sehemu nne tofaudi duniani kwa wakati mmoja.  

Tunapotangaza baa la njaa inamaanisha kwamba Maisha ya watu wengi tayari yameshapotea. Endapo tutasubiri kubaini hilo kwa hakika watu wengi watakuwa tayari wameshakufa.” 

Baa la njaa ile hali ya kuwa na njaa iliyokithiri kwa mujibu wa madaraja yanayofafanua kuhusu viwango vya njaa (IPC) ambayo yanatumiwa na mashirika ya kibinadamu kuelezea viwango vya kutokuwa na uhakika wa chakula kuanzia daraja la 1 hadi la 5.