Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Soko la mpakani Tanzania na Burundi ni daraja kwa ukuaji wa jamii hizo jirani 

Soko la Kakonko nchini Tanzania mpakani na Burundi.
UNCDF/Video
Soko la Kakonko nchini Tanzania mpakani na Burundi.

Soko la mpakani Tanzania na Burundi ni daraja kwa ukuaji wa jamii hizo jirani 

Ukuaji wa Kiuchumi

Biashara kati ya taifa moja na nyingine ni sehemu ya taswira ya kiuchumi na kijamii ya nchi nyingi barani Afrika na hususan maeneo ya mipakani. Na hali hiyo ndio inayoshuhudiwa mjini Kigoma mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Muhange na Muhange juu ni vijiji viwili vilivyoko takriban kilometa 46 magharibi mwa mji wa Kakonko mkoani Kigoma nchini Tazania mpakani na Burundi ambako katika kipindi cha miaka mingi kumekuwa na soko linalowavutia wafanya biashara kutoka wadi na wilaya jirani. 

Ni kwa kutambua umuhimu wake sasa shirika la maendeleo ya mitaji la Umoja wa Mataifa, UNCDF na halmashauri ya wilaya ya Kakonko wameanzisha soko kubwa zaidi linalovuka mipaka ya nchi hizo mbili ambalo linalenga kuwaleta pamoja wafanya biashara takriban elfu tatu, wakiwemo wakulima, wafugaji na watoa huduma, hali ambayo italeta mabadiliko chanya katika wilaya ya kakonko Tanzania na jimbo la Cacunzo Burundi lakini pia kwingineko.Nehamus Paulo ni afisa mkuu Muhange juu, "Makusudi kwanza ya kupata hili soko linaitwa soko la ujirani mwema hicho ndio kitu cha kwanza, kwa hilo soko hili litakuwa la wananchi wa Tanzania na wananchi wa Burundi. Kwa hiyo moja itakuwa ni fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na wa Burundi kubadilishana mawazo kibiashara na kuwezeshana kibiashara kwa kutumia soko hili."

Wengi wa wafanyabiashara wanaosubiri kukamilika kwa soko hilo ni wanawake kwani karibu asilimia 60 ya vibanda na maduka yatatolewa kwa ajili ya kundi hilo, mmoja wa wanawake hao ni Yoranda Msio anasema, "Soko tulilokuwa tunalitumia hapo chini huwa tunaweka bidhaa zetu chini, wakati wa mvua tunahangaika, ubora wa vile vitu tunavyoviuza unapungua mara vinakuwa vichafu, vinaloa. Kwa wale wenye watoto walikuwa wanapata shida sana kwani mtoto atajigaragaza kwenye uchafu, atakusumbua anaenda anashika, anaharibu. Ujio wa hili soko mimi nimelifurahia bidhaa zangu hazitakuwa chafu. Misukosuko ya kujitwisha kila siku mzogo itapungua maana nikilieata bidhaa zangu hapa nikiuza zikibaki zitaaa hapa na zitalindwa."

Mapato kutokana na biashara ndogo ndogo ni kiungo muhimu katika kupunguza umasikini na kukuza uchumi kama anayoafiki Asteria Msonge mchumi kutoka wilaya ya Kakonko, "Kipato chao kitaongezeka kati ya asilimia kumi hadi ishirini kwa mwezi ukiacha yale mapato ya ujumla ya Kijiji cha Muhange na Muhange juu. Ujio wa soko hili utaongezeka urahisi wa kukusanya mapato na pamoja na kuongezeka kwa mapato yenyewe ukilinganisha na soko la awali.”