Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Côte d'Ivoire: UN yalaani machafuko na kutaka kuheshimiwa kwa katiba 

Uhesabu wa kura katika kituo Abidjan baada ya uchaguzi 2015.  Côte d’Ivoire ni moja ya nchi zilizotzjwa katika ripoti ya IPU.
Photo: UNOCI (file)
Uhesabu wa kura katika kituo Abidjan baada ya uchaguzi 2015. Côte d’Ivoire ni moja ya nchi zilizotzjwa katika ripoti ya IPU.

Côte d'Ivoire: UN yalaani machafuko na kutaka kuheshimiwa kwa katiba 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani machafuko nchini Côte d'Ivoire na kutoa wito wa kuheshimiwa kwa katika katika taifa hilo la Afrika Magharibi. 

Tume huru ya uchaguzi nchini humo CEI jana Jumanne asubuhi ilitangaza matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyomtaja Rais anayetoka Allasane Ouattara kuwa ndio mshindi wa uchaguzi wa Urais uliofanyika Oktoba 31. 

Sasa matokeo hayo ya awali ni lazima yathibitishwe na baraza la katiba la nchi hiyo. 

Bwana Guterres amesema anafahamu kuhusu tangazo hilo lililotolewa na CEI la matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais ambayo yanapingwa na upande wa upinzani. 

Nchi hiyo imekuwa katika machafuko kwa miezi kadhaa ambayo hata baada ya tangazo la matokeo la CEI hayajapungua. 

“Katibu Mkuu amelaani vikali machafuko ambayo yametokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Ameshtushwa na kupotea kwa Maisha ya watu wengi na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika” amesema msemaji wa Umoja wa Mataifa katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo. 

Kwa mujibu wa duru za Habari watu 9 wameuawa katika machafuko tangu upigaji kura siku ya Jumamosi. 

Machafuko hayo pia yamewalazimisha raia wengi wa taifa hilo kukimbilia katika nchi jirani. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema zaidi ya watu 3200 wamepata hifadhi nchini Liberia, Ghana na Togo.