Haki za wabunge wa upinzani zinakiukwa sana wakati wa uchaguzi:IPU 

4 Novemba 2020

Muungano wa kimataifa wa mabunge IPU umesema umepokea madai mapya ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wabunge wa upinzani katika nchi ambazo zinafanya uchaguzi na umetoa wito wa madai hayo kuchunguzwa haraka na kupatiwa ufumbuzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya IPU iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis madai hayo yanahusisha wabunge wa upinzani na haki zao za msingi za uhuru wa kujieleza , kukusanyika na kutembea ambao umeelezwa kubinywa hususan nchini Venezuela, Côte d’Ivoire na Tanzania. 

Madai hayo ni miongoni mwa kesi zinazohusisha wabunge takriban 300 kutoka nchi 19 ambayo yalipokelewa na kamati ya haki za binadamu ya IPU na kufanyiwa tathimini na kamati hiyo na kisha kutoa mapendekezo kwa baraza la IPU. 

Taarifa hiyo ya IPU imesema baadhi ya ukiukwaji wa haki unaodaiwa kufanywa ni pamoja na utesaji, vitisho vya kuuawa, ukatili wa kingono na mazingira ya mrundikano kwa wabunge ambao wanashikiliwa rumande hivi sasa. 

Mfano nchini Venezuel IPU imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoathiri wabunge 134 kutoka vyama vya muungano wa upinzani wakati huu wa maandalizi ya uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Desemba 6 ambapo inadaiwa wabunge karibu wote hao wameshambuliwa, kutishiwa, kudhalilishwa au kunyanyaswa na wafuasi wa serikali. 

Nchini Côte d’Ivoire IPU inatathimini kesi za wabunge 9 wa upinzani ambao haki zao za msingi zimekiukwa ikiwemo kukamatwa kiholela na kuswekwa rumande. 

Nako Tanzania IPU inafanyia tathimini Ushahidi mpya wa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya mbunge wa zamani na mgombea mkuu wa upinzania katika uchaguzi wa Rais uliofanyika karibuni, bwana Tundu Lissu. 

IPU inasema taarifa ilizozipokea zinasema Bwana Lissu amekuwa akilengwa na vitisho vya kuuawa pamoja na ukiukwaji mwingine katika wiki za kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28. 

IPU imeitaka mamlaka nchini Tanzania kuchunguza jaribilio la kuuawa, madai ya vitisho vya kuuawa na manyanyaso mengine dhidi ya Bwana. Lissu. 

IPU imeongeza kuwa inatiwa hofu na kuongezeka kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wabunge wa upinzani katika sehemu mbalimbali duniani na imekuwa ikiwasiliana na mamlaka za nchi husika ili kusaka suluhu ya haraka dhidi ya madai hayo. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter