Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD yasaidia wanawake wa Mouradi, Niger kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Baadhi ya maeneo ya Niger yameharibiwa kutokana na matumizi mabaya ya ardhi yasiyo endelevu.
©FAO/Giulio Napolitano
Baadhi ya maeneo ya Niger yameharibiwa kutokana na matumizi mabaya ya ardhi yasiyo endelevu.

IFAD yasaidia wanawake wa Mouradi, Niger kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Nchini Niger, mfuko wa maendeleo ya kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD kwa kushirikiana na serikali unasaidia wazalishaji wadogo wa nafaka hususani vikundi vya wanawake katika eneo la Mouradi ambao mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri sana maisha yao ili waweze kukabiliana na hali inayobadilika na pia majanga ya baadaye.

Wakati msimu wa mavuno ulipoisha, mashamba yalibaki bila kitu, na kinyume na miaka mingine, haya ni mavuno ya pekee kwa mwaka mzima kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyofanya wakazi wa eneo la Mouradi nchini Niger kushuhudia ukame mkali.  

Na sasa watu wanategemea nafaka hizo tu walizozivuna katika msimu mmoja. Aisha Moussa na wakulima wengine wadogo wadogo kama yeye wanatarajia siku zijazo zisizo na uhakika. Aisha anasema, “mabadiliko ya tabianchi yameathiri mavuno. Mwaka jana tulipata mvua za kwanza mwezi Mei, na mwaka huu zimenyesha mwezi Agosti. Na ikaathiri kiwango cha mavuno. Hakukuwa na maji ya kutosha.” 

Hali ya ukame katika maeneo haya ya katikati mwa ukanda wa Sahel, tayari kwa muda mrefu yanasababisha ugumu. Baadhi ya maeneo haya yanashuhudia joto kali zaidi duniani na misimu mifupi ya mvua isiyotabirika inaathiri zaidi ya watu milioni 100 ndiyo maana IFAD kwa kushirikiana na serikali na makundi ya wanawake wa maeneo haya wanajaribu kuwasaidia vikundi vya wanawake kuweza kukabiliana na hali hii. 

Ghala limejengwa hivi karibuni ili kutunza nafaka ambazo familia zitahitaji kwa ajili ya matumizi katika kipindi ambacho hakuna mavuno. Na baada ya wanawake hawa kupewa mafunzo kuhusu masuala ya fedha, wanawake wenyewe ni wasimamizi wa shughuli hii. Zaidi ya wanawake 2000 sasa wamejifunza kuandika, kusoma na uhasibu. Kwa kutumia ujuzi huu wanaweza kupanga na kuweka akiba kwa ajili ya siku zijazo, jambo ambalo linamaanisha fedha yao inaweza kutumika katika kipindi kirefu cha ukame. 

Kipindi cha nyuma wanawake hawa kama Aisha walikuwa wanauza mazao yao kwa bei ya chini kwa kuwa walikuwa hawawezi kufika kwenye masoko makubwa. Lakini sasa barabara iliyotengenezwa ya takribani kilomieta 458 inawasaidia kufika kwenye soko na kuuza mavuno yao ya ziada llililofadhiliwa na IFAD na hivyo kujiongezea kipato kinachowasaidia kulisha familia zao. Aisha anasema, “kwa fedha taslimu nitanunua pilipili, viungo, chumvi, Mafuta na nitavipeleka kijijini kupika na kuuza nikiwa nyumbani.” 

Uzuri katika soko hili la kisasa, bei zinawekwa wazi kwa jamii kujionea, kwa hivyo hakuna anayeweza kumpunja mwingine.