Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake ni kichocheo cha ujenzi wa amani Colombia- Naibu Katibu Mkuu Amina

Wanawake nchini Colombia wakipamba kwa ujumbe wa amani mji wa Monterredondo
UN Verification Mission in Colombia/Daniel Sandoval
Wanawake nchini Colombia wakipamba kwa ujumbe wa amani mji wa Monterredondo

Wanawake ni kichocheo cha ujenzi wa amani Colombia- Naibu Katibu Mkuu Amina

Wanawake

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa kinawa mkataba wa kihistoria wa amani wa Colo,mbia wa mwaka 2016 ili kuwezesha jamii zenye mnepo wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.
 

Bi. Mohammed amesema hayo mwishoni mwa ziara yake nchini Colombia, ziara ambayo ameifanya kwa njia ya mtandao, na kugusia zaidi umuhimu wa kujikita zaidi kwenye maeneo ya vijijini ambayo yameathiriwa zaidi na COVID-19 na ghasia.
“Ni muhimu kujenga fursa mpya za maendeleo, kuimarisha usalama na kusisitiza uwepo wa mamlaka ya nchi kwenye taifa ambalo limekumbwa na machungu na sasa janga la Corona,” amesema Bi. Mohammed mwishoni mwa ziara hiyo ya kimtandao.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J.Mohammed akishiriki ziara ya kimtandao Colombia akiwa kwenye ofisi yake jijini New York, Marekani
UN /Mark Garten
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J.Mohammed akishiriki ziara ya kimtandao Colombia akiwa kwenye ofisi yake jijini New York, Marekani

Amesema huu ni wakati wa kufiria upya hatua za kujenga tena upya, kutomwacha yeyote nyuma ili kufanikisha amani endelevu.

Amekumbusha katika kutekeleza jukumu hilo kubwa, dhima ya wanawake ni muhimu akiongeza kuwa miaka minne baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani, wanawake wanaendelea kuwa vichocheo nyuma ya utekelezaji wa mkataba huo.

Wanawake wajenzi wa amani

Naibu Katibu Mkuu pia amefanya ziara ya kimtandao kwenye eneo la Vista Hermosa, eneo lililoko kusini-mashariki mwa Colombia ambalo liliathiriwa zaidi na mzozo wa muda mrefu nchini humo.

“Tulikuwa na fursa ya kutembelea Vista Hermosa kukutana na wanawake vijana wajenzi wa amani ambao waliathirika zaidi na mzozo wa kivita lakini wameazimia kusaka amani na utu wa jamii zao,” amesema Bi. Mohammed.

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko na mshikamano katika utekelezaji wa mkataba wa amani, “ambao tunatambua haukosi changamoto, ili kusaidia kuchochea utangamano wa kiuchumi na kijamii.”

Bi. Mohammed pia alikutana na wanawake watetezi wa haki za binadamu na viongozi wanawake na kujadili maendeleo na changamoto za kutekeleza mkataba wa amani.

Ametiwa moyo na ujasiri na mnepo wa mashirika ya wanawake na viongozi wa wanawake ambao wameendelea kuwa kichocheo cha ujenzi wa amani na ukosefu wa usalama.

Usawa wa Jinsia katika kujikwamua na COVID-19

Naibu Katibu Mkuu alikuwa pia na mkutano kwa njia ya video na Rais Iván Duque ambapo walijadili athari za kiuchumi na kijamii za janga la Corona na jinsi ya kuwalinda wale walio hatarini zaidi na kuchagiza ukwamukaji jumuishi, endelevu na usioharibu mazingira.

Mama na mwanawe wakiwa hospitalini nchini Colombia akati huu wa janga la COVID-19
PAHO
Mama na mwanawe wakiwa hospitalini nchini Colombia akati huu wa janga la COVID-19

Bi. Mohammed amepongeza azma ya Colombia ya kusaka usawa wa kijinsia na juhudi zake za kuhakikisha wanawake ni kitovu cha harakati za kujikwamua kutoka COVID-19 na utekelezaji wa mkataba wa amani.

Ziara hiyo ya kimtandao pia ilionesha kazi za Umoja wa Mataifa Colombia, sambamba na ushirikiano na mamlaka za kitaifa na kimkoa na mashirika ya kiraia, ikiwemo hatua za kukabili janga la Corona na changamoto za kuimarisha amani.

Ziara ya kwanza ya kimtandao tangu mlipuko wa COVID-19

Ziara hii ya tarehe 28 hadi 29 Oktoba mwaka 2020 ni ya kwanza ya kimtandao kuwahi kufanyika tangu janga la Corona.

Ziara hiyo imeonesha umuhimu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama ambalo limetimiza miaka 20 mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu katika ziara hiyo ya kimtandao aliambatana na Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi Mtendaji wa  UN-Women; Rosemary DiCarlo Mkuu wa Idara ya Siasa na Ujenzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa na;  Pramila Patten,  Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu katika masuala ya ukatili wa kingono kwenye mizozo.  

Mara ya mwisho Bi. Mohammed kufanya ziara kamilifu Colombia ilikuwa mwaka 2015 wakati wa uzinduzi wa kamisheni ya kitaasisi ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.