Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Thamani ya jamii mijini imedhihirika wakati wa COVID-19:UN

Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi. Tarehe 9 mwezi Agosti mwaka huu wa 2022 wananchi wa Kenya wanapiga kura.
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi. Tarehe 9 mwezi Agosti mwaka huu wa 2022 wananchi wa Kenya wanapiga kura.

Thamani ya jamii mijini imedhihirika wakati wa COVID-19:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika kuelekea siku ya miji duniani hapo kesho Oktoba 31, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe maalum wa siku hiyo amesema miji imebeba gharama kubwa ya janga la corona au COVID-19 lakini jamii katika miji hiyo zimedhihirisha thamani yake katika kukabiliana nalo na kuongeza kuwa 

“Katika siku hii ya miji duniani tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na jamii za mashinani katika majiji na miji. Maeneo ya mijini tayari ni maskani ya asilimia 55 ya watu wote wa dunia na idadi hii inatarajiwa kukua hadi asilimia 68 ifikapo 2050. Ukuaji wa haraka wa miji yetu lazima uweze kukabiliana ipasavyo na janga hili na kujiandaa na milipuko yoyote ya magonjwa siku za usoni.” 

Amesema wakati COVID-19 ikiathiri kwa kiasi kikubwa afya ya umma na huduma za msaada, jamii zimeshirikiana na serikali katika mapambano ya janga hilo na kwamba ,“Tumeshuhudia majirani wakinunua bidhaa na kuwapikia wagonjwa na wazee, wakazi wakiwashangilia na kuwahamasisha wahudumu wa afya, huku watu wa kujitolea na makundi ya kidini yakiwasaidia walio hatarini. Jamii ni bunifu, zina mnepo na zinajituma, na zina jukumu kubwa katika kujenga miji endelevu kiuchumi, kijamii na kimazingira, hebu na tuendelee kutambua thamani yao.” 

Amesisitiza kuwa jamii zikishirikishwa katika sera na ufanyaji maamuzi matokeo yake ni makubwa. Naye Mkurugenzi mtendaji wa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif katika ujumbe wake wa siku hii amesema ,“Tunahitaji kutambua kwamba jamii zinapaswa kuwa kitovu cha kuunda suluhu za muda mrefu za miji yao na lazima tuzisikilize kwani uzowefu wao utasaidia kujenga miji yenye mnepo na usawa siku za usoni na kuthamini mchango wa jamii ni hatua muhimu katika kuelekea mabadiliko tunayohitaji kujijenga vyema upya.” 

Siku ya miji duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 31 na mwaka huu kaulimbiu ni “kuthamini jamii na miji yetu”