Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka Ghana hadi Ugiriki, nimejifunza mengi, sasa nataka kusaidia wengine- Zachariah

Zachariah, mhamiaji kutoka Ghana anayeishi nchini Ugiriki.
Video ya UNICEF
Zachariah, mhamiaji kutoka Ghana anayeishi nchini Ugiriki.

Kutoka Ghana hadi Ugiriki, nimejifunza mengi, sasa nataka kusaidia wengine- Zachariah

Wahamiaji na Wakimbizi

Mtoto mhamiaji kutoka nchini Ghana ambaye sasa anaishi nchini Ugiriki amesema kutokana na yale aliyopitia, safari ngumu ya kunusurika kifo na sasa angalau anaona mwanga mwishoni mwa tanuru, amejizatiti kusaka elimu na ufahamu ili hatimaye asaidie watoto wengine kwa kuwa anafahamu maana ya maisha ya kukosa.

Zachariah, mwenye umri wa miaka 18 huyu raia kutoka Ghana, kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, anatoa nasaha kuwa saka elimu na ufahamu badala ya utajiri, kwa kuwa dunia ya leo inabadilika kila uchao, na ufahamu utakuwezesha kumudu maisha na si utajiri.

Kauli hii ya Zachariah inazingatia historia yake! Anasema, “nilitoka Ghana kuja Ugiriki nikiwa na umri wa miaka 16. Kwa kuwa nilikuwa peke yangu, hakukuweo mtu wa kunitunza. Safari haikuwa rahisi kabisa. Nakumbuka nililala porini kwa siku tatu bila chakula wala maji. Msafirishaji haramu akaniambia nipande boti bila jaketi la uokozi. Asubuhi iliyofuatia nilifika Ugiriki na ilikuwa mchanganyiko wa furaha na huzuni pia kwa sababu niliepuka kifo.”

Zachariah, kutoka Ghana akiwa katika shule ya kijamii ya kimarekani mjini Athens nchini Ugiriki.
Video ya UNICEF
Zachariah, kutoka Ghana akiwa katika shule ya kijamii ya kimarekani mjini Athens nchini Ugiriki.

Maisha yalikuwa mazuri na hadi alipata fursa ya kujiunga na shule lakini ujio wa ugonjwa wa Corona au COVID-19 mwaka huu ulibadili maisha ya Zachariah ambaye sasa ana umri wa miaka 18. Alipata msongo wa mawazo na hofu iwapo akiugua nani atamtunza kwa kuwa hana familia.

Zachariah anasema ili kuondoa fikra hizo nilianza mazoezi kila siku. Nilijifunza kupitia mtandao. Ninaishi na wenzangu watatu, wakiondoka asubuhi napata muda wa kusoma. Halikadhalika usiku pia nasoma.

Pindi anapotakiwa kuwa darasani, Zacharian anakwenda shuleni na licha ya yote anayopitia ana ndoto akisema, "kuna kitu moja natakuwa kuwa! Nataka kuwa na shirika langu la kusaidia watoto ili waweze kuwa na hamu ya kujiletea mabadiliko na kujiamini ya kwamba hakuna tumaini linalopotea. Nimejifunza kutoa na kusaidia wengine, si kwa sababu ni tajiri, la hasha! Kwa sababu nimepitia hali ya kutokuwa na kitu."

Zaidi ya yote, Zachariah amesema ametambua kuwa hakuna hali ya kudumu duniani na hivyo anatambua kuwa hata COVID-19 itapita punde na ataendelea vyema na elimu yake. Ujumbe wake ni kwamba “jiamini kwamba unaweza kufanya kitu fulani.”