Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto katika nchi maskini wamepoteza miezi minne ya masomo tangu kuanza kwa janga la COVID-19-Ripoti 

Wanafunzi waliporejea darasani katika shule ya msingi San Pedro Kusini Magharibi mwa Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejo
Wanafunzi waliporejea darasani katika shule ya msingi San Pedro Kusini Magharibi mwa Côte d'Ivoire.

Watoto katika nchi maskini wamepoteza miezi minne ya masomo tangu kuanza kwa janga la COVID-19-Ripoti 

Utamaduni na Elimu

Watoto wa shule katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati chini, tayari wamepoteza takribani miezi minne ya masomo tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona ikilinganishwa na wiki sita za upotezaji masomo katika nchi zenye kipato cha juu. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa hii leo mjini New York na Washington Marekani pamoja na Paris Ufaransa na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO na la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na  Benki ya Dunia. 

Robert Jenkins ambaye ni Mkuu wa Elimu katika UNICEF amesema, "hatuna haja ya kuangalia mbali ili kuona uharibifu ambao umefanywa na janga hilo kwa watoto wa shule kote ulimwenguni. Katika nchi za kipato cha chini na cha kati chini, uharibifu huu unakuzwa kutokana na  uwezo mdogo wa kuweza kusomea nyumbani, hatari zilizoongezeka za kupunguzwa kwa bajeti na mipango iliyocheleweshwa katika kufungua tena shule imezuia nafasi yoyote ya kawaida kwa watoto wa shule. Kipaumbele cha kufungua shule na kutoa mafunzo yanayohitajika ni muhimu sana.” 

Ripoti hiyo inakusanya matokeo kutoka katika utafiti mbalimbali juu ya hatua ya kitaifa ya elimu kwa COVID-19 iliyofanywa katika takribani nchi 150 kati ya mwezi Juni na Oktoba mwaka huu. Watoto wa shule katika nchi za kipato cha chini na cha kati chini walikuwa na uwezekano mdogo wa kupata ujifunzaji wa nje ya shule, uwezekano mdogo wa kufuatiliwa kuhusu upotezaji wao wa kujifunza, uwezekano mkubwa wa kuwa na ucheleweshaji kwa shule zao kufunguliwa na wana uwezekano mkubwa wa kuhudhuria shule zilizo na rasilimali duni ili kuhakikisha undeshwaji salama. 

“Wakati zaidi ya theluthi mbili ya nchi zimefungua shule zao kikamilifu au kwa sehemu, nchi 1 kati ya 4 wameshindwa kufungua shule katika tarehe walizokuwa wamepanga na hawajapanga tarehe mpya, nyingi ya nchi hizo zikiwa zile za kipato cha chini na kati chini.” Inaeleza ripoti hiyo ya UNESCO, UNICEF na Benki ya Dunia.    

Ni nchi 1 tu kati ya nchi 5 zenye kipato cha chini ziliripoti kuwa siku za masomo ya nje ya shule ni sawa tu na kama siku rasmi shuleni, ikilinganishwa na robo tatu ya nchi kote duniani.  

Vilevile ripoti imebainisha kuwa kati ya nchi 79 ambazo zilijibu maswali yanayohusiana na fedha, karibu asilimia 40 ya nchi zenye kipato cha chini na cha kati chini tayari wameona au wanatarajia kupungua kwa bajeti ya elimu ya nchi zao kwa mwaka wa sasa wa fedha au ujao. 

Matokeo mengine ya utafiti yameonesha kuwa karibia nchi zote zilijumuisha ujifunzaji kutokea nyumbani kwa njia ya mtandao, Televisheni na redio pamoja na vifurushi kutoka shuleni kwenda kwa watoto majumbani. Nchini 9 kati ya 10 ziliwezesha upatikanaji wa ujifunzaji mtandaoni, mara nyingi kupitia simu za kiganjani au kwa kusaidia upatikanaji wa mfumo wa intaneti kwa gharama nafuu au pasipo gharama lakini hali hii ilikuwa inatofautiana kati ya nchi na nchi.