Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu 2 wa kutoa chanjo dhidi ya Polio Somalia wauawa, UNICEF yalaani

Mtoto akisubiri chanjo wakati wa kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya Polio na Surua kwenye mji mkuu wa Mogadishu nchini Somalia mwezi Septemba mwaka huu wa 2020.
WHO Somalia/Ismail Taxta/Ildoog
Mtoto akisubiri chanjo wakati wa kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya Polio na Surua kwenye mji mkuu wa Mogadishu nchini Somalia mwezi Septemba mwaka huu wa 2020.

Wahudumu 2 wa kutoa chanjo dhidi ya Polio Somalia wauawa, UNICEF yalaani

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limeeleza kushtushwa kwake na mauaji ya wafanyakazi wawili wa kibinadamu mjini Mogadishu nchini Somalia hii leo.

Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia, Jesper Moller amesema katika taarifa iliyotolewa leo Mogadishu ya kwamba "watu hao wawili majasiri wakitoa chanjo dhidi ya Polio walikuwa mstari wa mbele wakiweka rehani maisha yao kwa ajili ya kutoa huduma za msingi kwa watoto walio hatarini zaidi."

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafanyakazi hao.

Bwana Moller amekumbusha kuwa mashambulio dhidi ya wahudumu wa kibinadamu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na katu hayawezi kuvumiliwa.

"UNICEF inalaani vikali shambulio hilo la kiuoga na inatoa wito kwa mamlaka za Somalia kuchunguza kwa kina tukio hilo," amesema Bwana Moller akiongeza kuwa wahudumu wa kibinadamu hawapaswi kuwa walengwa.

Kwa mujibu wa WHO, wahudumu hao wa kibinadamu nchini Somalia, pamoja na kutekeleza wajibu wao wa kutoa chanjo dhidi ya Polio, wanaratibu pia harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa kufuatilia na kutembelea vituo vya afya na kupitia taarifa zinazotolewa na maafisa wa polio wa wilaya kuhusu janga la Corona.