Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru ya amani yaanza kuonekana katika eneo la PK 5, MINUSCA yashuhudia 

Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui
UN photo / Catianne Tijerina
Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui

Nuru ya amani yaanza kuonekana katika eneo la PK 5, MINUSCA yashuhudia 

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani na utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya kati MINUSCA, umewapongeza waliokuwa wanachama wa makundi ya wapiganaji katika eneo la PK 5 waliokuwa wanajiita makundi ya kujilinda baada ya kukabidhi silaha zao mbele ya Waziri wa nchi hiyo anayesimamia upokonyaji silaha kutoka kwa raia, ujumuishaji na urejeshaji katika jamii wa watu waliokuwa wapiganaji ikiwa ni sehemu za Umoja wa Mataifa kuhamasisha usitishaji mapigano duniani kote.

Ni katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, wakati wa hafla ya uzinduzi wa awamu ya nne ya kupunguza vurugu za jamii chini ya usimamizi wa MINUSCA

Kwa mwendo wa taratibu, askari wanamuongoza Mohamed Rahama, msemaji wa kundi la kujihami kwa silaha ambaye amebeba silaha kali ya kivita, akielekea kumkabidhi Waziri Maxime Mokom kama ishara ya usitishaji mapigano katika eneo la PK 5 ambalo kwa muda limeshuhudia mapigano na ukatili kati ya makundi yenye misimamo ya kidini.  

Msemaji huyo wa kundi la wapiganaji Bwana Mohamed Rahama anapokabidhi silaha, anatamka maneno akisema, "tunaacha sasa ufyatuaji silaha. Tunaamini katika hili. Tunataka amani irejee katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.” Waziri Mokom anaipokea silaha kwa mikono miwili kama alivyokabidhiwa. 

Bunduki nyingine nzitonzito za kivita zilizosalimishwa zimetandazwa chini zikileta matumaini ya amani.  

Baada ya kuzipokea silaha, Waziri Maxime Mokom, anasema,"Sote tunafurahi leo kuona kaka na dada zetu wa PK 5 wakichukua hatua ya kuja kwa hiari kukabidhi silaha zao na kwa hivyo kugeuza ukurasa wa unyanyasaji wa kijamii." 

Jumla ya silaha 14 za kivita, silaha ziliyotengenezwa kienyeji, maroketi manne na makombora, na risasi 104, zimekabidhiwa kama ishara na vikundi 14 vya zamani vya kujilinda vya PK5. 

Msemaji wa kundi, Bwana Rahama baada ya kuwa amekabidhi silaha sasa anazungumza na waandishi wa habari akisema, “Tulikuwa na nia ya kuweka silaha chini muda mrefu uliopita. Kwanza, tulianza kujenga mshikamano wa kijamii na mwenzetu waliokuwa katika kundi la Anti Balaka. Na hii ndio awamu ya pili. Tayari tusalimisha silaha chache. Inamaanisha kwamba kweli tuko kwenye njia ya amani.” 

Mkuu wa kitengo katika MINUSCA cha usalimishaji silaha na urejeshaji katika jamii wa waliokuwa wapiganaji Pierre Emmanuel Ubalijoro, alikuwepo kushuhudia na anasema,"nimefurahishwa na ishara hii ya leo. Inaonesha kwamba kweli kuna kujitolea kwenda kuelekea kwenye amani katika jamii ya PK 5. Na kwa niaba ya MINUSCA, na uongozi wa MINUSCA, nakupongezeni na kukuhimizeni msonge mbele." 

MINUSCA, kupitia mpango wake unaojulikana kama CVR wa kupunguza vurugu za kijamii,  inaunga mkono serikali ya Afrika ya Kati katika juhudi za kuleta utulivu kwenye eneo la PK5, eneo ambalo linakaliwa na  Waislam wengi Bangui, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishambuliwa na vikundi vyenye silaha vinavodai kuwa vinajilinda.