Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira na makazi salama vyawaacha wafanyakazi wahamiaji hatarini Lebanon:IOM 

Mama mkulima akipanda mbegu za mimea katika shamba ndogo Akkar, kaskazini mwa Lebanon.
UNDP Lebanon/Dalia Khamissy
Mama mkulima akipanda mbegu za mimea katika shamba ndogo Akkar, kaskazini mwa Lebanon.

Ukosefu wa ajira na makazi salama vyawaacha wafanyakazi wahamiaji hatarini Lebanon:IOM 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema ukosefu wa ajira endelevu na makazi salama kutokana na janga la corona au COVID-19 na athari zake za kiuchumi vimewaacha maelfu ya wafanyakazi wahamiaji nchini Lebanon katrika hatari kubwa ya usafirishaji haramu wa binadamu na ukatili.

Kwa mujibu wa taarifa ya IOM iliyotolewa leo mjini Beirut, milipuko miwili iliyotokea mjini humo Agosti 4 mwaka huu imefanya hali kubwa mbaya zaidi na kufanya maelfu ya wafanyakazi wahamiaji kukosa ajira na kutokuwa na njia ya kurejea nyumbani. 

IOM inakadiria kwamba takriban wahamiaji 24,500 mjini Beirut wamepoteza kazi zao, makazi yao au kuathirika kwa njia moja au nyingine na milipuko ya Beirut. 

Kuna jumla ya wafanyakazi wahamiaji 400,000 nchini Lebanon wengi wao wakitokea Ethiopia, Ufilipino, Kenya, Sierra Leone na Bangladesh. 

IOM inasema wafanyakazi hawa wamekuchukua hatari kubwa kufanyakazi Lebanon kwa matumaini ya kulipwa dola zitakazowawezesha kuzisaidia familia zao nyumbani walikotoka. 

Shirika hilo linasema wahamiaji wengi walifika Lebanon kupitia mfumo wa Kafala ambao ni mradi wa ufadhili wa ajira unaotumiwa na nchi nyingi za Mashariki ya Kati, huku ufadhili huo ukiwasaidia kupata vibali vya kusafiria, vya ajira na vya kuishi nchini Lebanon. 

Hata hivyo IOM inasema ingawa mfumo huo lengo lake ni zuri la kufungua mlango wa ajira kwa wahamiaji lakini pia unawaweka wahamiaji hao hatarini kwa kuwapa mamlaka makubwa waajiri wao ambao wengi huwapokonya passi za kusafiria wafanyakazi hao na kufanya kuwa vigumu kwao kuondoka. 

Hali mbaya ya uchumi nchini Lebanon imewafanya waajiri wengi kushindwa kuwalipa ujira wafanyakazi hawa na kuwatumbukiza wengi katika madeni, kushindwa kulipa kodi ya pango, kukosa chakula na mahitaji mengine ya msingi na kubwa zaidi IOM inasema wameshindwa kutuma fedha nyumbani kwa familia zao. 

Shirika hilo limeongeza kuwa wahamiaji wengi wametimuliwa kwenye nyumba walizopanga na kulazimika kulala mitaani na wengine kujikusanya na kulazimika kupanga chumba kimoja hali inayowaweka katika hatari kubwa ya maambukizi ya COVID-19

Hivi sasa mashirika mengi ya kibinadamu ikiwemo IOM wanahofia kuendelea kukosa ajira kwa wafanyakazi hawa wahamiaji kutawaweka katika hatari nyingine kubwa ya usafirishaji haramu wa binadamu.