Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yashtushwa na kulaani mauaji ya raia Cameroon

Hali ya kukosekana kwa utulivu, imekuwa ikiendelea katika eneo linalotumia lugha ya kiingereza nchini Cameroon
UN OCHA/GILES CLARKE
Hali ya kukosekana kwa utulivu, imekuwa ikiendelea katika eneo linalotumia lugha ya kiingereza nchini Cameroon

UN yashtushwa na kulaani mauaji ya raia Cameroon

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea kushtushwa kwake na ripoti ya kwamba shule moja kwenye mji wa kumba kusini magharibi mwa Cameroon ilishambuliwa tarehe 24 mwezi huu huu na watoto kadhaa kuuawa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani, imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa katika tukio hilo watoto wengine kadhaa walijeruhiwa na kwamba “shambulio hilo la kuchukiza ni kumbusho juu ya gharama kubwa ambayo raia wakiwemo watoto wanalipa huku wakinyimwa haki yao ikiwemo elimu. Mashambulio dhidi ya maeneo ya shule lazima yakome kwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.”

Bwana Guterres ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za watoto waliopoteza maisha na huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Amesihi mamlaka za Cameroon zifanye uchunguzi wa kina ili wahusika wa shambulio hilo wafikishwe mbele ya sheria.

Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa pande zilizojihami zijizuie kufanya mashambulizi dhidi ya rai ana ziheshimu sheria za kimataifa za kibindamu na za haki za binadamu.

Bwana Guterres amesihi kwa dhati pande zote kuitikia wito wake wa sitisho la mapigano duniani huku akisema kuwa, “Umoja wa Mataifa upo kusaidia mashauriano jumuishi yanayoweza kuleta suluhu ya kudumu kwenye mzozo huko kaskazini-magharibi mwa Cameroon.”

Mzozo wa Cameroon

Duru za habari zinasema kuwa kile kilichoanza kama harakati za raia wa kusini mwa Cameroon kusaka usawa zimeongezeka na kuwa janga kamili ambapo vikundi vya waasi vinavyosaka kumaliza kile kinachodaiwa kuwa udhibiti wa wacameroon wanaozungumza lugha ya kifaransa kwenye maeneo ya wacameroon wanaozungumza lugha ya kiingereza vimebeba silaha dhidi ya vikosi vya serikali.

Mapigano hayo yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha huku makumu ya maelfu wakilazimika kukimbia makazi yao.

Viwanda vimechomwa moto, barabara hazipitiki, bohari za kuhifadhi bidhaa zimeteketezwa, huku madereva wa malori wakiwa wanatekwa mara kwa mar ana watekaji kudai fedha ili wawaachie huru.