Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa UN wa kutokomeza nyuklia kuanza kutumika Januari mwakani: Guterres asema ni hatua ya kipekee

Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo, picha hii ilipigwa  umbali wa kilometa 3 kutoka kitovu cha bomu hilo.
UN /Nagasaki International
Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo, picha hii ilipigwa umbali wa kilometa 3 kutoka kitovu cha bomu hilo.

Mkataba wa UN wa kutokomeza nyuklia kuanza kutumika Januari mwakani: Guterres asema ni hatua ya kipekee

Amani na Usalama

Hatimaye mkataba wa kimataifa wa kupinga matumizi ya silaha za nyuklia, TPNW, utaanza kutumika tarehe 22 mwezi Januari mwaka ujao wa 2021 baada ya Honduras kuwa mwanachama wa 50 wa Umoja wa Mataifa kuridhia mkataba huo jana jumamosi, hatua ambayo imeelezewa kuwa zama mpya ya kutokomeza silaha za nyuklia duniani.

 

Kufuatia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa taarifa yake akipongeza mataifa yote yaliyoridhia  mkataba huo ambao ulipitishwa na mataifa 122 kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2017, akisema hatua yao na ile ya mashirika ya kiraia zimesaidia kupiga marufuku silaha hizo hadi sasa.

Miongoni mwa makundi ya kiraia yaliyoongoza kampeni kufanikisha mkataba huo ni Kampeni ya kimataifa ya kutokomeza silaha za nyuklia, ICAN, ambao walishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2017 ambapo Mkurugenzi Mtendaji wake Beatrice Fihn amesema kuanza kutumika kwa mkataba huo ni sawa na kufungua sura mpya ya kuondokana na silaha za nyuklia. Miongo ya uanaharakati umefanikisha kile ambacho wengi walisema hakiwezekani: Kupiga marufuku silaha za nyuklia.

Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani  ya UN, jijini New York, Marekan
UN/Jihye Shin
Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani ya UN, jijini New York, Marekani

Mmoja wa manusura wa shambulio la bomu la atomiki huko Hiroshima nchini Japan mwaka 1945, Setsuko Thurlow aliiambia ICAN kuwa  amejitolea maisha yake yote kutokomeza nyuklia, “sina cha kusema zaidi ya shukrani kwa wale wote waliofanya kazi kufanikisha mkataba huo.”

Hatua ya kihistoria ya Jumamosi imefikiwa siku moja baada ya Jamaica na Nauru kuwasilisha nyaraka zao za kuridhia mkataba huo ikimaanisha kuwa ndani ya siku 90, mkataba huo utaanza kutumika na kupiga marufuku silaha za nyuklia, ikiwa ni zaidi ya miaka 75 tangu zilipotumika mara ya kwanza mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Shukrani kwa manusura

 “Kuanza kutumika kwa mkataba huu ni shukrani kubwa kwa manusura wa milipuko na majaribio ya silaha za nyuklia, wengi wao wakiwa wachechemuzi wa mkataba huu,” amesema Bwana Guterres.

Ameelezea kuwa kuanza kutumikwa kwa TPNW ni ukomo wa harakati za dunia za kuonesha madhara ya matumizi ya silaha za nyuklia.

“Inawasilisha azma ya maana ya kuondokana kabisa na silaha za nyuklia, azma ambayo inasalia kuwa kipaumbele cha juu cha Umoja wa Mataifa katika udhibiti kuenea kwa silaha.”

Amesema kwa sasa anasubiria kwa hamu kutekeleza jukumu lake la kuwezesha mkataba huo sasa katika utokomezaji kabisa wa silaha za nyuklia.

Orodha ya nchi zinazomiliki silaha za nyuklia na idadi ya silaha hizo.
UNODA
Orodha ya nchi zinazomiliki silaha za nyuklia na idadi ya silaha hizo.

Hadi sasa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia ambazo ni MArekani, Uingereza, Urusi, China na Ufaransa bado hazijatia saini mkataba huo.

Mkataba ulipitishwa tarehe 7 mwezi Julai mwaka 2017 wakati wa Mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ukiwa ni mkataba wa kwanza wa kimataifa wenye nguvu kisheria katika kuzuia kuenea kwa nyuklia katika miongo miwili.