Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko UN kwa kuepusha COVID-19 kwenye ulinzi wa amani- Balozi Gastorn

Gari la kivita la kubeba askari likivuka daraja huko Beni, DR Congo.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Gari la kivita la kubeba askari likivuka daraja huko Beni, DR Congo.

Heko UN kwa kuepusha COVID-19 kwenye ulinzi wa amani- Balozi Gastorn

Amani na Usalama

Tanzania imepongeza hatua za sekretarieti ya Umoja wa Mataifa za kuweka mikakati ya kuhakikisha ulinzi wa walinda amani na raia dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
 

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn amesema hayo Ijumaa wakati akihutubia kikao cha kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Balozi Gastorn katika hotuba yake hiyo ya kurasa 8 amesema, “tunashukuru sana na tunampongeza Katibu Mkuu kwa hatua za kina zilizochukuliwa na sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ikiwemo kujengea uwezo unaohitajika wa kitabibu na marekebisho yanayotakiwa kwa vikosi vyote vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Mataifa duniani kote ili kuepusha COVID-19 dhidi ya walinda amani na raia wanaowalinda.”

Akizungumzia hatua za kupunguza  ukubwa wa vikosi vya ulinzi wa amani, hatua zinazotekelezwa hivi sasa kutokana na ukata unaokabili Umoja wa Mataifa, Balozi Gastorn amesema, “tunasihi wadau wote wahakikishe kuwa hatua zozote za kurekebisha au kupunguza ukubwa wa vikosi hivyo lazima zifanyike baada ya kuzingatia taarifa sahihi kwenye eneo husika ili kuepusha kuhatarisha maisha ya askari na raia wasio na hatia.”

Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kuhakikisha kuwa kila mara wanakuwa na mawasiliano na nchi zinazotoa askari na wanajeshi na vyombo vya kikanda ili kuhakikisha kuwa majukumu yanapangwa vyema ili vikosi vinavyopangwa kwenye eneo husika viweze kushughulikia changamoto zilizopo.

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.
TANZABATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.

UN na mawasiliano kwa umma

Mwakilishi huyo wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akaangazia pia masuala ya mawasiliano kutoka Umoja wa Mataifa kwenye kwa umma ambapo amepongeza Idara ya Mawasiliano ya Umma ya chombo hicho, DGC akisema inajitahidi kufikia maeneo ya ndani kusambaza taarifa kuhusu utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, ulinzi wa amani na masuala ya kibinadamu.

Hata hivyo ameibua hoja kadhaa zenye lengo la kuimarisha upashaji huo wa habari ili uwe kwa kina zaidi.
Mathalani amesema, “ijapokuwa vituo vingi vya habari vya Umoja wa Mataifa, UNIC vimeanzisha ushirikiano na ubia bora na serikali na vyombo vya habari  kwenye nchi husika, bado ufikiaji wake mashinani una changamoto. Ndio maana tunataka DGC ije n mfumo bora wa kuwezesha umma kupata habari na kushiriki zaidi. Wito huu unahitaji kuimarisha uwezo wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ambayo kwa sasa ina watendaij 3 wenye mkataba kuongezewa muda ilhali mwingine 1 ni mkataba wa muda, ilhali wanatakiwa kuwa na watendaji 7 wa mkataba wa kuongezewa muda kama ilivyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka 2011.”

Halikadhalika amependekeza UNIC Dar es salaam iongezewe rasilimali watu ili iweze kufanya kazi yake ipasavyo wakati huu ambapo amesema ingawa lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji zaidi ya milioni 500, bado haijapata hadhi yake hivyo anapendekeza hatua za kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Mataifa kando ya Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kiarabu, Kispanyola na Kirusi.

Balozi Gastorn amesema lugha ya Kiswahili hivi sasa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika na hivi karibuni imepitishwa kuwa moja ya lugha rasmi za jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC.

Ametamatisha akisema kuna umuhimu wa kujumuisha nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili katika orodha ya wanaoweza kushiriki katika mpango wa vijana wabobezi, YPP, ili kujenga uwezo wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.