Uhusiano mpya kati ya Sudan na Israel utasongesha amani Mashariki ya Kati- Guterres

24 Oktoba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema amepokea ripoti ya kwamba Sudan imekubali kurejesha uhusiano wa kawaida na Israel, huku akitumaini ya kwamba ushirikiano zaidi utasongesha amani na ustawi duniani.
 

Taarifa ya Katibu Mkuu imekuja baada ya makubaliano yaliyoratibiwa na Marekani na kutangazwa rasmi na Rais Donald Trump siku ya Ijumaa, wakati wa mazungumzo kwa njia yake kwa njia ya simu mawaziri wakuu wa Sudan na Israel katika Ikulu ya Marekani.

Katika wiki zijazo, wajumbe kutoka Sudan na Israel watakutana ili kuhitimisha vipengele vya makubaliano hayo.

Kama sehemu ya makubaliano, Marekani itaiondoa Sudan kutoka katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi, na kuruhusu misaada na uwekezaji wa kiuchumi kuingia katika taifa hilo ambalo sasa liko kwenye kipindi cha mpito wa kidemokrasia baada ya kupinduliwa kutoka madarakani Rais Omar al-Bashir mwaka jana.

Kwa sasa Sudan inajiunga na Falme za kiarabu na Bahrain ambazo nazo zimerejesha uhusiano na Israel wiki chache zilizopita, kupitia usuluhishi wa Marekani, na kuwa nchi za kwanza kutambua Israel katika zaidi ya miongo miwili.

Kihistoria, Sudan imepigana vita dhidi ya Israel mwaka 1948 na 1967 na kwa mujibu wa vyombo vya habari, imekubali kulipa mamilioni ya dola ili kufidia manusura wa mashambulizi yaliyofanywa na Al Qaeda kwenye balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998, wakati ambao kikundi hicho makao yake makuu yalikuwa Sudan.

UN imeazimia kusaidia Sudan

Guterres katika taarifa yake ameelezea matumaini kuwa makubaliano hayo yatasongesha ushirikiano zaidi na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashra na kuleta fursa mpya za kusongesha amani na ustawi wa kiuchumi  kwenye pembe ya Afrika na Mashariki ya Kati.

“Umoja wa Mataifa unasalia kidete kusaidia juhudi za Sudan za kukwamuka kiuchumi na kijamii na ustawi kwa wananchi wote wa Sudan na ukanda mzima,” amesema Guterres.

Wakati huo huo, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov ameungana na Bwana Guterres katika kupongeza makubaliano hayo akisema yatachochea  ushirikiano na kuleta fursa mpya siyo tu pembe ya Afrika bali pia eneo zima la Mashariki ya Kati.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud