Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN ikitimiza miaka 75 leo, malengo ya kuanzishwa ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule- Guterres

Picha ya mtoto mwenye furaha akiwa kwenye kituo cha kulea watoto kilichoko wilaya ya Iganga nchini Uganda.
UNICEF/Proscovia Nakibuuka
Picha ya mtoto mwenye furaha akiwa kwenye kituo cha kulea watoto kilichoko wilaya ya Iganga nchini Uganda.

UN ikitimiza miaka 75 leo, malengo ya kuanzishwa ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule- Guterres

Masuala ya UM

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa chombo hicho mwaka 1945 huko San Francisco nchini Marekani wakati huu wanachama waanzilishi wakiwa ni 50.

Hii leo chombo hicho kina jumla ya wanachama 193 ambapo katika ujumbe wake mahsusi kwa siku hii, Katibu Mkuu Antonio Guterres  amesema lengo la kuanzisha Umoja wa Mataifa ni muhimu hivi sasa kuliko wakati wowote ule.

Kusongesha utu wa kibinadamu, kulinda haki za binadamu, kuheshimu sheria za kimataifa na kuepusha binadamu dhidi ya vita.

Amesema kuwa pindi janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 lilipotikisa dunia, alitoa wito wa sitisho la mapigano.

Vijana wa Bor jimboni Jonglei nchini Sudan Kusini wakivuna mazao kutoka kwenye shamba wanamopatiwa mafunzo na walida amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini
UNMISS
Vijana wa Bor jimboni Jonglei nchini Sudan Kusini wakivuna mazao kutoka kwenye shamba wanamopatiwa mafunzo na walida amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini

“Katika dunia yetu hii leo, tuna adui mmoja, COVID-19. Sasa ni wakati wa kuimarisha na kusongesha harakati za amani ili kufanikisha sitisho la mapigano. Muda unakimbia.  Lazima tuwe na amani na sayari yetu. Dharura ya tabianchi inatishia sayari yetu,”  amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa ni lazima kuhamasisha dunia nzima ili kuondokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050.

Bwana Guterres amesema nchi nyingi zaidi na kampuni zinaahidi kufikia lengo hilo.

Duniani kote lazima tuchukue hatua zaidi ili kutokomeza machungu yatokanayo na umaskini, ukosefu wa usawa, njaa, chuki na tupige vita ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, jinsia au tofauti yoyote ile 

“Miezi hii ya janga la Corona imeshuhudia ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake na wasichana,” amesema Katibu Mkuu.

Kuhusu harakati za kusaka chanjo amesema “lazima tuendeleze pale tulipofikia. Ushirikiano wa kipekee wa kimataifa unaendelea ili kuweza kupata chanjo ya bei nafuu na itakayofikia watu wote ili kukabili COVID-19,”  amesema Bwana Guterres.

Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

UN na SDGs

Kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, Katibu Mkuu yanatoa matumaini ya kukwamuka kwa hali bora zaidi.

“Tunakabiliwa na changamoto kubwa. Lakini kwa ushirikiano wa kimataifa na mshikamano tunawea kuzikabili. Ndio sababu ya kuwepo kwa Umoja wa Mataifa.,” amefafanua Katibu Mkuu akiongeza kuwa katika siku hii ya Umoja wa Mataifa, “nasihi watu popote pale walipo waungane. Umoja wa Mataifa siyo tu uko kwa ajili yenu bali ni wa kwenu na ninyi ndio Sisi watu wa dunia.”

Katibu Mkuu amesema kwa pamoja “hebu tuzingatie maadili ya Chata ya Umoja wa Mataifa. Hebu na tuendelezee kwenye mafanikio yaliyopatikana kwenye miongo yote. Hebu na tufanikishe dira yetu ya pamoja kwa dunia bora kwa wote.”

Mkutano wa kupitisha Chata ya Umoja wa Mataifa huko San Francisco kuanzia Aprili 25 hadi 26 mwaka 1945
UN
Mkutano wa kupitisha Chata ya Umoja wa Mataifa huko San Francisco kuanzia Aprili 25 hadi 26 mwaka 1945

Kuundwa kwa UN

Chata ya Umoja wa Mataifa ilitiwa saini tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945 na wawakilishi kutoka nchi 50 waasisi. Poland ambayo haikuwa na mwakilishi kwenye mkutano wa San Francisco, ilitia saini Chata hivyo baadaye na hivyo kufanya nchi wanachama wa mwanzoni kufiia 51.

Umoja wa Mataifa ulianza kazi rasmi tarehe 24 Oktoba mwaka 1945 pindi Chata hiyo iliporidhiwa na China, Ufaransa, Shirikisho la nchi za kisovieti, USSR, Uingereza na Marekani na idadi kubwa pia ya nchi zingine zilizoridhia.

UN na mtazamo kutoka kwa wakazi wa nchi wanachama

Mwezi Januari mwaka huu wa 2020, Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres alizindua mjadala wa kimataifa ukihoji watu kupitia ukusanyaji maoni juu ya matumaini yao na hofu yao kwa mustakabali na vipaumbele vyao kuhusu ushirikiano wa kimataifa.

Matokeo ya utafiti yamezingatiwa na viongozi wa dunia na yaliwezesha kupitishwa kwa azimio la kisiasa wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha mjadala wa wazi wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu. Azimio hilo linatokana na mchakato uliofanywa na serikali chini ya maudhui Mustakabali tuutakao, Umoja wa Mataifa tunaouhitaji: kusisitiza azma yetu ya pamoja ya ushirikiano wa kimataifa.