Najiona nina bahati sana kuzaliwa mwaka mmoja na Umoja wa Mataifa – Balozi Mongela

23 Oktoba 2020

Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, wapo pia wananchi katika nchi 193 ambao nao pia walizaliwa mwaka mmoja na Umoja huo mwaka 1945. 

Miongoni mwao ni Balozi Getrude Mongela kutoka Tanzania ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995, halikadhalika Rais wa Bunge la Afrika na pia kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya taifa lake na pia kuliwakilisha nje ya nchi. 

Stella Vuzo wa kituo cha habari za Umoja wa Mataifa UNIC  jijini Dar es salaam, Tanzania amezungumza naye ambapo amesema, “kwanza nafikiria kuwa mimi Mungu amenipendelea jamani, nitazaliwaje mwaka mmoja na Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo wakati mwingine nasema ni baraka za mwenyezi Mungu na jinsi Umoja wa Mataifa unavyozidi kujiimarisha, na mimi nataka niendelee kujiimarisha.” 

 Balozi Mongela amesema alipotimiza miaka 75 mwezi Septemba mwaka huu, hakutazama umri wake bali aliangalia amefanya nini katika miaka 75 akakuta amefanya mambo mengi, “nimesoma, nimeongoza, nimezaa, nimeolewa, mimi nadhani nimejitahidi. Sijui sasa tunaposubiri mwezi Oktoba na wenzangu Umoja wa Mataifa niwaulize nyie wenzetu mmefanya nini, lakini wenyewe nadhani historia ya walichofanya ni kubwa.” 

Akizungumzia mwelekeo wake, amesema yeye huwa anaishi kwa awamu kwa hiyo ameamua kupanga miaka mitano ijayo nini atakachofanya ili jamii iweze kufanya inamkumbuka kwa jambo gani, “kwa hiyo miaka mitano ijayo ni muhimu kwangu. Ni miaka ambayo sitatizama umri bali nitatizama uwezo wa kufanya nini.” 

Kipindi gani muhimu cha ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa? 

Stella alimuuliza Balozi Mongela ni muda upi ulikuwa muhimu sana wakati akifanya kazi na Umoja wa Mataifa ambapo amesema, “moja ninachokumbuka ni pale waliponipatia nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wa mkutano wa nne wa kimataifa wa wanake huko Beijing nchini China, na wakati huo huo walinipatia cheo cha kuwa naibu msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo ilikuwa nafasi ya kukaa na kupika sera na siasa za Umoja wa Mataifa.  Mimi nadhani kwa Umoja wa Mataifa walinipa nafasi nzuri sana. Natumaini nimeitumia vizuri kujaribu kuleta mabadiliko katika uhusiano kati ya wanawake na wanaume.” 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter