UNMISS yatoa mafunzo kwa jeshi la Sudan Kusini kuzuia ukatili wa kingono 

23 Oktoba 2020

Ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa malengo ya Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake  miaka 75 ya uwepo wake,  kuwa mtetezi mkubwa wa amani na haki za wanadamu kote duniani, nchini Sudan Kusini, mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS umeshirikiana na Jeshi la wananchi wa Sudan Kusini SSPDF kuwapa mafunzo wakufunzi kuhusu kuzuia ukatili wa kingono unaohusiana na mizozo.

Majenerali wa jeshi la wananchi wa Sudan Kusini, wanawake kwa wanaume, wamekaa ukumbini, kwa makini wanamsikiliza afisa wa ulinzi wa wanawake kutoka UNMISS akitoa maelezo kuhusu kuzuia ukatili wa kingono unaohisiana na mizozo.  

Wakati vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipoanza nchini humo mnamo mwaka 2013, wanawake na wasichana wadogo walikuwa kati ya waathirika wakubwa  zaidi wa ukatili wakati miili yao ilipofanywa kuwa sehemu ya uwanja wa vita. Miaka saba baadaye, nchi mpya zaidi ulimwenguni iko kwenye hatua ya hatimaye kuweza kujiimarisha kama demokrasia ya kweli na makubaliano ya amani na hatua zinazochukuliwa kuunda jeshi la kitaifa lenye umoja, hata hivyo, mengi yanahitajika kufanywa ili kuhakikisha kuwa haki na utu wa wanawake na wasichana unasimamiwa kila wakati ndio maana mafunzo kama haya ni muhimu. Mafunzo ambayo yanawafunza wakufunzi kuhusu kuzuia ukatili wa kijinsia unaohusiana na mizozo ili nao wakawafunze wengine. Shailesh Tinaiker ni Kamanda wa kikosi katika UNMISS anasema, "kama askari, wacha niwe wazi juu ya jambo moja - hakuna askari ana haki ya mali ya mtu yeyote, hana haki ya kuchukua uhai wa mtu yeyote asiye na hatia, hana haki ya kukiuka utu wa mwanamke yeyote au kusababisha kitendo cha vurugu kwa mtoto yeyote. Hili ni jukumu la msingi la kila askari, iwe uko upande wa kushinda au uko upande wa kupoteza." 

UNMISS\Nektarios Markogiannis
Waathirika wa unyanyasaji wa kingono wanaendelea kuhangaika kupata huduma za kutosha za matibabu na afya ya akili nchini Sudan Kusini.

 

Makamanda wamesikiliza, wameshiriki na wamechangia maoni yao. Kisha, Huma Khan, Mshauri Mkuu wa ulinzi wa wanawake katika UNMISS anaeleza mafunzo hayo yalivyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa Sudan Kusini yenyewe,"Sudan Kusini imekuwa na historia ya unyanyasaji wa kingono unaohusiana na mizozo tangu mwaka 2013. Ni nchi ambayo imeorodheshwa katika ripoti za kila mwaka za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wakati eneo linapoorodheshwa kunakuwa na ushahidi wa kuaminika dhidi yao kwamba wanahusika katika kutumia unyanyasaji wa kingono. Orodha hii inaleta vizuizi kadhaa kwa nchi na njia ya kujiondoa ni kutafuta fursa za mafunzo na Umoja wa Mataifa kwa jeshi la nchi hiyo, kuwa na mpango kazi na kuchukua hatua madhubuti za kushughulikia tatizo hili, na kuonesha kwamba wako tayari kulishughulikia.” 

Lengo kuu la mafunzo ni kuhamasisha mazungumzo yenye maana juu ya mipango ya hatua iliyopo ya kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa kuimarisha uwajibikaji ndani ya jeshi la wananchi wa Sudan Kusini, SSPDF na kuhamasisha kila mwanachama juu ya majukumu ya kitaifa na kimataifa katika kulinda raia dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter