Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipimo cha haraka cha COVID-19 jawabu mujarabu kwa Afrika

WHO imeanza kusambaza barani Afrika kitendanishi cha kupima kwa haraka virusi vinavyosababisha COVID-19.
WHO/Africa
WHO imeanza kusambaza barani Afrika kitendanishi cha kupima kwa haraka virusi vinavyosababisha COVID-19.

Kipimo cha haraka cha COVID-19 jawabu mujarabu kwa Afrika

Afya

Uwezo wa nchi za bara la Afrika upimaji virusi vya Corona, COVID-19 utaongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya kuruhusiwa kuanza kutumika kwa kitendanishi kinachowezesha majibu kupatikana haraka.
 

Kitendanishi hicho kimethibitishwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, amesema Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao hii leo huko Brazaville, Congo.

Nchi za Afrika zimekuwa zikihaha kupima wananchi wake virusi vya Corona ambapo ni mataifa 12 katika ukanda huo wameweza kufikia kiwango cha kupima wananchi 10 kati ya 10,000.

Dkt. Moeti amesema kuongezeka kwa kasi ya upimaji COVID-19 Afrika kutaleta mapinduzi makubwa ya hatua za bara hilo katika kukabili gonjwa hilo ambalo hadi sasa halina tiba wala chanjo bali hatua za kujikinga.

Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda
© UNICEF
Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda

WHO inasema ingawa baadhi ya nchi za Afrika zinaongoza kwa kupima wananchi wake kwa kiasi kikubwa, mathalani Senegal, lakini bado kiwango cha upimaji hakifikii taifa lenye ukubwa sawa kama vile Uholanzi.

Je ni kipimo gani kinatumia hivi sasa?

WHO inasema kwa sasa nchi nyingi zinatumia kiimo cha Polymaerase Chain Reaction au PRC, ambacho kinahitaij maabara, vitendanishi na wataalamu, na hivyo kusababisha uchunguzi kufanyika katika maeneo ya mijini pekee.

Kipimo hicho kinapotumiwa, mgonjwa anasubiri saa 48 au hata zaidi ya siku 10 kupata majibu kwa kuwa yanapelekwa maabara kwa ajili ya uthibitisho.

Kipimo cha sasa ni rahisi kutumia na ni bei nafuu kuliko PCR na kinatoa majibu kati ya dakika 15 hadi 30 na hivyo kuwezesha ugatuzi kwenye upimaji wa virusi hivyo.

“Nchi nyingi za Afrika zimejikita katika kupima wasafiri, wagonjwa na waambata wao, na tunakadiria kuwa kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa COVID-19 bado hawajabainika kutokana na kutopimwa. Kwa kutumia kipimo hiki cha haraka, mamlaka zinaweza kuongeza kasi yao dhidi ya COVID-19 hata kwenye mazingira magumu kama vile maeneo yenye msongamano na jamii za ndani zaidi,” amesema Dkt. Moeti.

Hata hivyo WHO imesema kuwa, vitendanishi hivyo vya upimaji haraka ni nyongeza tu katika aina ya mfumo wa upimaji wa PCR na kwamba siyo mbadala.

Vipimo hivyo viwili vinachunguza protini kwenye mwili wa binadamu protini inayozalishwa na virusi vya Corona aina ya SARS-CoV-2, virusi ambavyo vinasababisha COVID-19.

Kinachochukuliwa katika mwili wa binadamu ni majimaji kutoka puani kwa kutumia pamba na kisha kuweka kwenye kikaratati ambako kuna rangi inayotoa majibu.

Je kipimo hiki cha majibu ya haraka kitumike wapi?

WHO inapendekeza maeneo manne: Mosi pale kwenye shaka na shuku ya mlipuko na ambako hakuna kipimo cha PCR yakiwemo maeneo ambayo in magumu kufikika. Pili katika kufuatilia kiwango cha mlipuko kwenye maeneo ambapo kisa angalau kimoja kimebainika kupitia kipimo cha PCR, mathalani kwenye magereza. Tatu, kwenye makundi yaliyo hatarini zaidi kama vile wahudumu wa afya na nne, kwenye maeneo ambako kuna mlipuko mkubwa miongoni mwa jamii.

Duniani vipimo milioni 120 vya aina hii vinasambazwa kwa nchi za vipato vya kati na chini kupitia mfumo wa ACT ulioandaliwa na WHO na wadau ili kuongeza kasi ya kutengeneza, kuzalisha na kuwezesha kupatikana kwa vipimo na chanjo dhidi ya COVID-19.