Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaporomosha ununuzi wa nguo duniani, Asia-Pasifiki yaathirika zaidi 

Wanawake katika kiwanda cha nguo Hai Phong nchini Vietnam
© ILO
Wanawake katika kiwanda cha nguo Hai Phong nchini Vietnam

COVID-19 yaporomosha ununuzi wa nguo duniani, Asia-Pasifiki yaathirika zaidi 

Haki za binadamu

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limepunguza sekta ya ushonaji nguo huko ukanda wa Asia na Pasifiki  kutokana na kuporomoka kwa mauzo ya rejareja hasa kwenye nchi zinazonunua zaidi nguo kutoka ukanda huo, umesema utafiti mpya wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO uliotolewa Geneva, Uswisi.

Mjini Jerash nchini Jordan wafanyakazi wa sekta ya nguo kutoka Bangladesh, Syria na Jordan wakiwa katika kiwanda cha kushona nguo wakati huu ambapo gonjwa la COVID-19 na hatua za kudhibiti vimevuruga mnyororo mzima wa usambazaji wa bidhaa hizo na hivyo kuathiri wafanyakazi na kampuni. 

Mchumi mwandamizi wa ILO ofisi ya Asia na Pasifiki Christian Viegelahn, amesema  mauzo kutoka mataifa 10 yanayoongoza kwa kutengeneza nguo kwenye ukanda huo ambayo ni Bangladesh, Cambodia, China, India, Indonesia, Myanmar, Pakistan, Ufilipino, Sri Lanka na Vietnam yameporomoka kwa hadi asilimia 70 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020. “Kwa hiyo kile tulichokishuhudia katika muda mfupi, ni kufungwa kabisa kwa viwanda,  wafanyakazi wengi wamebakia bila kazi, na katika matokeo mengi, wengi hawana kipato, na vile viwanda ambavyo vinafunguliwa, haviendelei na uzalishaji kamili kama awali na baadhi ya wafanyakazi hawarejeshwi kazini. Kuna kupunguzwa kwa mishahara na kucheleweshwa kwa malipo, ni mambo ya kawaida.” 

Kwa kuangalia ni wafanyakazi gani wameathirika zaidi, Bwana Viegelahn amesema, “Sekta ya ushonaji nguo imeajiri zaidi wanawake. Kwa hiyo katika baadhi ya nchi, mwanamke mmoja kati ya watano anafanya kazi kwenye kiwanda cha nguo na tunaona baadhi ya dalili ambazo zinadhihirisha wazi ongezeko la pengo la usawa kati ya wanawake na wanaume.” 

Utafiti huo unataka hatua pana zaidi za kusaidia wafanyakazi na kampuni ikiwemo uratibu wa kimataifa wa mipango ya usaidizi na nafuu ya madeni