Nigeria komesheni ukatili wa polisi dhidi ya wananchi-UN 

21 Oktoba 2020

Viongozi wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa mamlaka nchini Nigeria kukomesha  ukatili wa polisi unaoripotiwa kufanyika dhidi ya wananchi. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani amelaani ongezeko la vurugu mnamo tarehe 20 Oktoba mwaka huu 2020 mjini Lagos ambazo zimesababisha vifo kadhaa na majeruhi. Aidha Guterres ametuma salamau za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia kupoana haraka wale waliojeruhiwa huku akizitaka mamlaka nchini humo kuchunguza matukio haya na kuwawajibisha wahusika. 

Bwana Guterres amevisihi vikosi vya usalama kuchukua hatua wakati wote kwa kujizuia wakati zaidi wakati pia akiwataka waandamanaji kufanya maandamano ya amani na kujiepusha na vurugu.  

“Katibu Mkuu anahimiza mamlaka kutafuta haraka njia za kurejesha amani. Anasisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi za kitaifa katika kutafuta suluhisho.” Imesema taarifa hiyo iliyosambazwa na Stephane Dujarric, ambaye ni Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.   

Kwa upande wake Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet hii leo mjini Geneva Uswisi amelaani vikali matumizi ya nguvu kubwa yanayofanywa na majeshi ya Nigeria mjini Lagos hususani jioni ya Jumanne wiki hii.  

Bi. Bachelet ametoa wito kwa mamlaka za Nigeria kuchukua hatua za haraka kushughulikia tatizo la msingi la ukiukaji unaoendelea kufanywa na vikosi vya usalama, na kufanya juhudi kali zaidi kuwafikisha mbele ya haki polisi na wanajeshi wenye hatia ya uhalifu dhidi ya raia.   

"Wakati idadi ya majeruhi wa mashambulizi ya risasi jana katika eneo Lekki huko Lagos bado haijulikani, kuna shaka kidogo kwamba haya yalikuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi, na kusababisha mauaji haramu na risasi za moto yaliyotekelezwa na vikosi vya jeshi vya Nigeria. Ripoti kwamba kamera za CCTV na taa zilizimwa kwa makusudi kabla ya risasi zinasumbua zaidi kwani, ikiwa inathibitishwa, zinaonesha kuwa shambulio hilo la kusikitisha kwa waandamanaji wa amani lilipangwa na kuratibiwa." Amesema Bachelet.  

 Raia wa Nigeria wanaandamana kupinga kitengo cha polisi ambacho awali kiliundwa kwa ajili ya kupambana na uhalifu lakini kwa madai yao kikosi hcho maarfu kama SARS kimegeuka kuwa genge la uhalifu ambalo linapora na kunyanyasa wananchi hususani vijana. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter