UN na jukumu la kuzuia na kusuluhisha migogoro 

21 Oktoba 2020

Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75 tareh 24 mwezi huu wa Oktoba, moja ya jukumu muhimu linalomulikwa ni nafasi yake katika kuzuia migogoro. 

Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, DPPA ndiyo yenye jukumu kubwa la kuratibu masuala ya uzuiaji wa migogoro katika nchi wanachama 193. 

Akizungumza katika video mahsusi kuhusu uzuiaji wa migororo wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa, Roselyne Akombe ambaye ni mkuu wa cha sera, miongozo na mafunzo katika kitengo cha sera na usuluhishi anasema “nchi wanachama zilipotia saini Chata ya kuanzisha Umoja wa Mataifa miaka 75 iliyopita, lengo lilikuwa ni kuepusha vizazi vijavyo dhidi ya Vita Kuu ya Tatu ya Dunia. Ililenga kuepusha mizozo. Kwa hiyo kuzuia migogoro kunasalia kuwa kipaumbele kikuu cha Umoja wa Mataifa.” 

Mambo ya kuzingatia kwenye uzuiaji migogoro 

Hata hivyo anasema inakuwa ni vigumu sana kwa watu wa nje kushawishi pande zinazozozana kuzungumza ili kusaka amani iwapo pande hizo hazitaki.  Lakini je uzuiaji wa migogoro unafanyika vipi? Idara hiyo inataja vipengele vikuu vitano ambavyo inasema ni muhimu ili kuweza kuzuia migogoro. 

Mosi, kufahamu hali halisi kwa kuwa na uelewa fika wa eneo husika na “na ndio maana tuna zaidi ya ofisi 65 maalum za kisiasa duniani kote kufanikisha hilo.” 

Pili ni kufuatilia mwenendo wa kisiasa mapema na hii ni kutambua fika pande zote husika, “siyo tu maafisa wa serikalini bali pi apande zote za jamii. Maafisa wetu wa dawati la kisiasa jijini New York, wanaohusika na nchi zote 193 wanachama, wanakuwa na uhusiano wa karibu na pande zote na kutoa uchambuzi wa mapema ili kufanikisha ushiriki wowote wa masuala ya kisiasa.”   

Tatu, ujumuishaji wa sauti za makundi yote kwenye jamii wakiwemo wanawake na vijana, nne ni ubia na mashirika ya kikanda na taasisi za kimataifa za kifedha na kuunganisha shughuli za muda mfupi za kisiasa na juhudi za muda mrefu za ujenzi wa amani na maendeleo. 

Kwa mujibu wa Bi. Akombe, hatua ya tano ambayo ni muhimu zaidi katika kuzuia mizozo ni utashi wa kisiasa kutoka pande zote. 

OCHA/Eve Sabbagh
Mvulana akienda kuchota maji katika kambi ya Minova ya wakimbizi wa ndani Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Nini madhara ya kushindikana kwa hatua hizo 5? 

Hata hivyo amesema pindi vipengele hivyo vitano vinaposhindikana, madhara yake yanakuwa ni dhahiri na ya kutisha. “Kama tulivyoshuhudia mwaka jana, mivutano katika chaguzi, maandamano na vipindi vya mpito vya kisiasa, kuna kazi kubwa siku za usoni.”  

Hata  hivyo amesema “sisi katika Umoja wa Mataifa hatukati tamaa na tumeazimia kuendelea kufanya kazi kwa bidii kuunga mkono juhudi za kitaifa, wanawake na wanaume duniani kote katika harakati zao za kuzuia migogoro.” 

UN Photo/Catianne Tijerina
Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui

Umoja wa Mataifa na usuluhishi wa migogoro 

Pindi migogoro inapoibuka katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, hatua zinafuatwa kusaka njia ya kupata suluhu kwa njia ya amani. 

Asif Khan ambaye mkuu wa usaidizi wa usuluhishi katika DPPA anafafanua kuwa jukumu la usuluhishi linalofanywa na Umoja wa Mataifa linahitaji mambo ya msingi ili liweze kufanikiwa. 

Nini mantiki ya usuluhishi? 

Kwa lugha ya kiingereza, wahusika wa usuluhishi hutambuliwa kama “Good Offices” ambapo Bwana Khan anasema, “ni usaidizi wowote wa tatu kwa pande zinazokinzana kwenye mzozo kwa lengo la kusaidia pande hizo kusuluhisha matatizo yao na inaweza kuwa katika njia mbalimbali.” 

Inaweza kuwa kushauri pande kinzani kwenye mzozo au serikali kama ilivyokuwa kwa Sudan au Sudan Kusini. Wakati mwingine kupeleka ujumbe baina ya pande zinazozozana au inaweza kumaanisha kujenga mawasiliano au kuaminiana kati ya pande zinazozozana bila hata upande wa tatu kushiriki moja kwa moja kwenye mchakato husika. 

Wakati mwingine inaweza kumaanisha kupatia utaalamu katika masuala mbalimbali ya mchakato wa amani. 

UN inapata wapi jukumu hilo? 

Umoja wa Mataifa inapata jukumu hilo la usuluhishi kutokana na dhima na uhalali wa Katibu Mkuu. Ni kutokana na jukumu  hilo ndipo linaibuka jukumu la usuluhishi.  

Umoja wa Mataifa unaamini kuwa usuluhishi unategemea ridhaa ya pande kinzani husika kwani bila hivyo, usuluhishi hauwezi kufanyika. 

Pande husika lazima zikubali upande wa tatu ushiriki katika usuluhishi. Msingi mkuu ni kutopendelea au kutogemea upande wowote. Msuluhishi naye ni lazima ajitahidi kuhakikisha kuwa mchakato mzima ni jumuishi, ili kila mtu – wanawake kwa wanaume, wenye ubia kwenye mchakato huo, wanashiriki. 

Kikubwa zaidi, pande husika lazima zimiliki mchakato wa usuluhishi, ikimaanisha umiliki wa kitaifa na msuluhishi lazima aheshimu sheria ya kimataifa na maadili na mifumo yote ya usuluhishi ikiwemo haki za binadamu. 

Tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kufikia amani yenye haki, jumuishi na endelevu. Na hili ni jambo ambalo msuluhishi anapaswa kutambua kuwa ndio lengo kuu.  

TAGS: Usuluhishi, Uzuiaji Mizozo, DPPA 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud