Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Fanyeni kazi kwa pamoja’ ili kukuza amani na usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi - Guterres

Mwanaume akiwa amembeba mtoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al-Dhale’e nchini Yemen.
YPN for UNOCHA
Mwanaume akiwa amembeba mtoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al-Dhale’e nchini Yemen.

‘Fanyeni kazi kwa pamoja’ ili kukuza amani na usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi - Guterres

Amani na Usalama

Kwa kuzingatia changamoto ngumu na anuwai katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ni muhimu kutafakari kwa kina zaidi juu ya jinsi jamii ya kimataifa hasa Baraza la Usalama linavyoweza kufanya kazi kwa umoja kukuza amani na usalama katika sehemu hii muhimu ya ulimwengu. Hiyo ni sehemu ya kwanza ya hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyoitoa kwa njia ya video kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ngazi ya mawaziri kuhusu utunzanji wa amani na usalama: mapitio ya kina kuhusu hali kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Bwana Guterres ameeleza kuwa anabakia kuwa na wasiwasi sana juu ya hali ya Yemen, mzozo wa ndani ambao umekuwa wa kikanda kwa muda.  

 “Takribani miaka sita ya vita imeharibu maisha ya mamilioni ya Wayemen na kudhoofisha juhudi za kujenga kujiamini katika eneo hilo. Nimetoa wito wa kusitisha mapigano ya haraka ulimwenguni ili kuzingatia vita moja ya kweli: vita dhidi ya janga la COVID-19. Baraza la Usalama limejiunga na wito huu. Lakini kama nilivyosema katika hotuba yangu kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tunahitaji kuongeza juhudi. Saa inazidi kuzunguka, na watu wanakufa. Yemen ni kidhibitisho cha kwanza cha hitaji la kutambua usitishajoi vita sasa.” Amesema Bwana Guterres.  

Wiki iliyopita ilileta mwangaza wa matumaini 

Katibu Mkuu Guterres amesema wiki iliyopita ilileta matumaini kwani pande kinzani zilichukua hatua ambayo inaleta matumaini kwa kuwaachia zaidi ya wafungwa 1,000, ambayo ni idadi kubwa kuachiwa tangu kuanza kwa mgogoro, “hatua hii si iliunganisha familia nyingi za Yemen na wapendwa wao, lakini pia ilionesha kuwa wahusika wana uwezo wa kufikia makubaliano na kufuata ahadi zao.” 

Umoja wa Mataifa unaendelea kuwezesha mazungumzo kati pande kinzani za Yemen kuhusu azimio la pamoja ambalo linajumuisha kusitisha mapigano kitaifa, hatua za kiuchumi na za kibinadamu na kuanza tena kwa mchakato wa kisiasa.