Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 6 anaishi katika umaskini uliokithiri-Utafiti 

Covid-19 imesukuma watu kutumbukia katika umasikini zaidi.
© UNICEF/Fazel
Covid-19 imesukuma watu kutumbukia katika umasikini zaidi.

Mtoto 1 kati ya 6 anaishi katika umaskini uliokithiri-Utafiti 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Tathimini ya utafiti uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na Benki ya Dunia iliyotolewa hii leo mjini New York na Washington DC Marekani imekadiria kuwa mtoto 1 kati ya 6 au sawa na watoto milioni 356 duniani kote, walikuwa wanaishi katika umaskini uliokithiri hata kabla ya janga la virusi vya corona, na hali inategemewa kuwa mbaya zaidi.

Utafiti wa ‘Makadirio ya Ulimwenguni ya Watoto katika Umaskini wa kifedha’ yamesema kuwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inachangia theluthi mbili ya watoto wanaoishi katika kaya ambazo zinahangaika kuishi kwa wastani wa dola 1.90 kwa siku au chini kwa kila mtu ambacho ni kipimo cha kimataifa cha umaskini uliokithiri. Asia Kusini inachangia takribani theluthi ya watoto hawa.   

Utafiti huo wa UNICEF na Benki ya Dunia unaonesha kuwa idadi ya watoto wanaoishi katika umaskini uliokithiri ilipungua kwa wastani wa watoto milioni 29 kati ya 2013 na 2017 lakini UNICEF na Benki ya Dunia wanaonya kuwa maendeleo yoyote yaliyofikiwa katika miaka ya hivi karibuni yanaenda polepole, yanasambazwa bila usawa, na yako hatarini kwa sababu ya athari za kiuchumi za janga la COVID-19

Sanjay Wijesekera ambaye ni Mkurugenzi wa mipango wa UNICEF anasema, “mtoto 1 kati ya watoto 6 anayeishi katika umaskini uliokithiri ni mtoto 1 kati ya 6 anayehangaika kuishi. Idadi hii pekee inapaswa kushtua mtu yeyote. Ukubwa na kina cha kile tunachojua kuhusu shida za kifedha zilizoletwa na jangala corona zimewekwa tu kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Serikali zinahitaji haraka mpango wa kupona kwa watoto ili kuzuia watoto wengi zaidi na familia zao kufikia viwango vya umaskini ambavyo havijaonekana kwa miaka mingi." 

Naye Carolina Sánchez-Páramo ambaye ni Mkurugenzi wa Kimataifa wa masuala ya umaskini na usawa wa Kimataifa wa Benki ya Dunia amsema, “ukweli kwamba mtoto mmoja kati ya sita alikuwa akiishi katika umaskini uliokithiri na kwamba asilimia 50% ya watu maskini waliokithiri ulimwenguni walikuwa watoto hata kabla ya janga la COVID-19 ni jambo la kutupa wasiwasi sana sisi sote. Umaskini uliokithiri huwanyima mamilioni ya watoto fursa ya kufikia uwezo wao, kwa ukuaji wa mwili na utambuzi, na kutishia uwezo wao wa kupata kazi nzuri wakiwa watu wazima. Kutokana na usumbufu mkubwa wa kiuchumi unaosababishwa na janga hilo, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kwamba serikali zisaidie kaya maskini zenye watoto sasa na kujenga tena mitaji yao ya kibinadamu wakati wa kupona.” 

Aidha utafiti wa UNICEF na Benki ya Dunia umeeleza kuwa umaskini uliokithiri kati ya watoto haujapungua kama vile ilivyokuwa kwa watu wazima; sehemu kubwa ya maskini ulimwenguni walikuwa watoto mnamo 2017, ikilinganishwa na ile ya 2013. Maeneo yote ya ulimwengu yalipata viwango tofauti vya kupungua kwa umaskini uliokithiri kati ya watoto, mbali na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo ilishuhudia ongezeko la idadi ya watoto milioni 64 wanaohangaika kuishi kwa dola 1.90 kwa siku, kutoka watoto milioni 170 mnamo 2013 hadi watoto milioni 234 mnamo 2017.