Kuelekea uchaguzi mkuu CAR, hali ya usalama bado ni ya wasiwasi 

Mankeur Ndiaye, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa CAR ambaye pia ni mkuu wa MINUSCA.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mankeur Ndiaye, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa CAR ambaye pia ni mkuu wa MINUSCA.

Kuelekea uchaguzi mkuu CAR, hali ya usalama bado ni ya wasiwasi 

Amani na Usalama

Ikiwa imesalia miezi miwili na nusu kufanyika uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, “hali ya kisaiasa bado ni ya wasiwasi na wagombea wengine tayari wanahoji uwezekano wa mkataba wa amani na hata kupendekeza kuujadili tena iwapo watachaguliwa.” Amelieleza leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Mankeur Ndiaye. 

Baraza la Usalama la Umaja wa Mataifa limefanya mkutano kuhusu CAR kwa kuzingatia hali ya kisiasa na usalama kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais, wabunge na serikali za mitaa uliopangwa kufanyika tarehe 27 mwezi Desemba mwaka huu wa 2020.  

Bwana Ndiaye amesema, "miezi ishirini baada ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Kisiasa wa Amani na Maridhiano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kati, kati ya  Serikali na vikundi 14 vyenye silaha, maendeleo muhimu yanaendelea kufanywa, hasa katika suala la mageuzi ya kisiasa, urejesho wa mamlaka ya serikali na haki ya mpito. ” 

Hata hivyo, Ndiaye ameonya juu ya hali ya "wasiwasi" ya kisiasa inayoendelea kabla ya uchaguzi. 

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umo wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba wagombea 16 wamesajiliwa kugombea nafasi ya urais wakiwemo wanawake watatu akiwemo Rais anayemaliza muda wake na “wagombea wengine tayari wanahoji uwezekano wa Mkataba wa Amani n ahata wanapendekeza kuujadili tena ikiwa watachaguliwa. Hivi karibuni muungano mkuu wa upinzani uliamua kutumia njia za kikanda kupinga uhalali wa marekebisho ya sheria ya Kanuni za Uchaguzi.” 

Bwana Ndiaye akatoa wito kwa wadau kuona chaguzi zijazo kama fursa ya kuimarisha mchakato wa kidemokrasia na kubadilisha kisiasa mgogoro ambao nchi inapitia kwa nia ya suluhisho la kudumu akisema, "ninaendelea kuhamasisha mazungumzo ya kisiasa kupitia ofisi zangu kusaidia kuunda mazingira yanayofaa kufanyika kwa uchaguzi unaojumuisha, uchaguzi huru, wa haki, uwazi, uaminifu na amani kwa kushirikisha jamii ya kimataifa, pamoja na G5 + na wahusika wa Afrika ya Kati huko Bangui.” 

Akiongea pia katika mkutano huo, Koen Vervaeke, Mkurugenzi Mtendaji wa Afrika wa Huduma za Nje za Muungano wa Ulaya amesema, "EU itaendelea kuwa mmoja wa wafuasi wenye nguvu wa mamlaka za Afrika ya Kati na wananchi katika juhudi zao za amani, upatanisho wa demokrasia ili kupona. Ili kufikia lengo hilo, tunahamasisha juhudi zetu zote: kisiasa, kibinadamu, maendeleo ya ushirikiano, usalama na usimamizi wa shida, ikiwa ni pamoja na kama ilivyotajwa dhamira mbili mpya za raia na IDP kuchangia Mageuzi ya Sekta ya Usalama." 

Kwa upande wake, Smail Chergui, Kamishna wa Amani na Usalama wa Muungano wa Afrika amesema "muungano wa Afrika unakaribisha sana ukombozi wa polisi wawili waliochukuliwa kama mateka na vuguvugu la 3R na inatoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wengine bado na bila masharti kifungoni. Inatia moyo kwamba vikundi vyenye silaha vinaendelea kuonyesha mtazamo mzuri katika kujaribu kuzuia mvutano na vurugu. Zaidi ya hapo awali, juhudi zote zinahitaji kuelekezwa katika kutekeleza Mkataba wa Amani. ” 

Ripoti ya Katibu Mkuu juu ya CAR ilibaini kuongezeka kwa vurugu, haswa kaskazini magharibi, ikisababisha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko CAR, MINUSCA kufanya operesheni kadhaa katika miezi ya hivi karibuni ili kusaidia kutuliza hali hiyo. 

 Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, takriban watu milioni 2.6 wanahitaji msaada wa kibinadamu katika CAR na watu milioni 2.36 wanachukuliwa kuwa hawana usalama wa chakula.