UNICEF kuandaa sindano na mabomba ya utoaji chanjo dhidi ya COVID-19

Wakati duniani inasubiri kwa hamu chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICF, nalo limeanza maandalizi ya kuhakikisha chanjo hiyo inatolewa na kusambazwa mapema na kwa usalama kwa kununua na kuhifadhi mabomba ya sindano na vifaa vingine vya kufanikisha zoezi hilo.
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa punde tu baada ya chanjo hiyo kukamilika majaribio yake na kuthibitika iko salama kwa matumizi, dunia itahitaji mabomba mengi ya sindano sambamba na dozi zenyewe.
Katika kuanza maandalizi hayo, UNICEF itahifadhi kwenye bohari zake mabomba milioni 520 ya sindano ili kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021 ina mabomba bilioni 1 kwa lengo ya kwamba mabomba yanayotakiwa yanafikia nchi zinazoyahitaji kabla ya chanjo kufika.
UNICEF inasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021, kwa kutarajia kuwa kuna chanjo za kutosha za COVID-19, shirika hilo linatarejia kusambaza zaidi ya mabomba bilioni 1 ya sindano kwa ajili ya utoaji wa chanjo ya COVID-19, ikiwa ni kando ya mabomba milioni 620 ambayo UNICEF itakuwa imenunua kwa ajili ya chanjo zingine kama vile surua na homa ya matumbo.
Akizungumzia mpango huo wa UNICEF, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Henrietta Fore amesema, “kupatia chanjo wakazi wa dunia dhidi ya COVID-19, itakuwa ni kazi kubwa katika historia ya binadamu, na tutahitaji kufanya kazi kwa haraka kadri chanjo hiyo inavyotengenezwa. Ili kwenda haraka, tunalazimika kuanza kazi hiyo kwa haraka sasa. Mwishoni mwa mwaka huu, tutakuwa tayari kuna mabomba nusu milioni ya kutolea chanjo yakiwa tayari yamehifadhiwa ambako yatasambazwa haraka na kwa gharama nafuu. Kiwango hicho kinatosha kwa kukidhi dunia mara moja na nusu.”
Kando mwa mabomba ya sindano, UNICEF pia inanunua makasha milioni 5 salama yatakayotumika kutupia mabomba na sindano zilizotumika kwenye vituo vya afya, lengo likiwa ni kuepusha majeraha yanayoweza kutokana na kuchomwa na sindano na pia kusambaza magonjwa kwa njia ya damu.
Kila kasha moja linachukua mabomba na sindano 100 na kwamba makasha hayo yanaweza kuhifadhiwa kabla ya matumizi kwa miaka 5.
Shirika hilo limesema kwa upande wa chanjo ili kuhakikisha inasafirishwa salama na katika kiwango cha joto kinachotakiwa, tayari kwa kushirikiana na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, wanapanga mpango wa kupata mifumo ya usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa kwa ubaridi kwa ubia na sekta ya umma na binafsi.