Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inatoa huduma ya afya ya akili kwa wakimbizi Kakuma, Kenya.  

Esperanza, mkimbizi, akiwa na wanawake wenzake katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma ,Kaskazini-Magharibi Kenya
Picha /Esperanza Tabisha
Esperanza, mkimbizi, akiwa na wanawake wenzake katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma ,Kaskazini-Magharibi Kenya

UNHCR inatoa huduma ya afya ya akili kwa wakimbizi Kakuma, Kenya.  

Afya

Kama sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya kibinadamu wameamua kutoa huduma ya afya ya akili kwa wakimbizi katika Kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

Huduma za afya ya akili ni muhimu lakini kwa takribani wakazi 200,000 wa kambi ya wakimbizi wa Kakuma nchini Kenya, ni vigumu kuipata huduma hiyo kirahisi. UNHCR na wadau wanatoa ushauri na huduma nyingine kama sehemu mapambano dhidi ya COVID-19, lakini fedha zaidi na msaada unahitajika kuhakikisha wakimbizi na wenyeji wao wanapata msaada wanaohitaji. 

Wakati wa janga la corona na hatua zilizofuata za kufungwa mipaka ambazo zilianza kutumika, washauri wa kisaikolojia wamekuwa wakitoa ushauri nasaha kwa watu wenye uhitaji, pamoja na wale walio katika vituo vya karantini na waliotengwa katika sehemu za uangalizi. Lynn Waithera ni mmoja wa wanasaikolojia wanaotoa ushauri kambini hapo Kakuma, “unakuta kuna watu wengi wa kuangaliwa. Kuna watu wengi wa kuhudumiwa, kuna watu wengi wa kutetewa, haswa linapokuja suala la afya ya akili na masuala ya kisaikolojia ambayo tunajua hata kutokana na COVID-19, idadi hiyo imeongezeka.” 

Msongamano wa watu katika kambi unaeleza picha ya wazi kuwa bila shaka wenye uhitaji pia ni wengi. Mwanasaikolojia Lynn Karanja anakutana nao ofisini hata mitaani ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa salama. Lynn anasema,“afya ya akili haianzi katika mashirika. Inaanzia nyumbani. Inaanza na hata jinsi tunavyojiangalia, jinsi tunavyoanza asubuhi. Tunachojiambia sisi wenyewe.” 

Yeye mwenyewe kwa kutambua kuwa tatizo la afya ya akili linaweza kupata yeyote kutokana na msongo wa mawazo unaoletwa na sababu mbalimbali, baada ya kazi Lynn Karanja anafuatilia mazoezi ya kutuliza mwili yanayotolewa na mmoja wa wakimbizi kambini hapo, "ni tatizo la ulimwengu mzima ambalo linaweza kushughulikiwa na kila mtu na mtu yeyote."