Kila la heri katika uchaguzi Guinea, jizuieni na machafuko:UN

Maisha ya kila siku mjini Conakry Guinea
World Bank/Dominic Chavez
Maisha ya kila siku mjini Conakry Guinea

 Kila la heri katika uchaguzi Guinea, jizuieni na machafuko:UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katika mkesha wa uchaguzi mkuu wa Rais nchini Guinea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote wa kitaofa nchini humo kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa ujumuishi na amani.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na msemaji wake mjini New York Marekani, Bwana Guterres ametoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao nchini Guinea kujizuia na vitendo vyovyote vya uchochezi, kauli za chuki, ubaguzi wa kikabila na machafuko.

Pia mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameyataka majeshi ya ulinzi na usalama ya nchi hiyo kuwajibika kwa uadilifu na kujizuia na matumizi ya nguvu kupita kiasi.

Kwa viongozi wa kisiasa na vyama vyao Katibu Mkuu amewasihi kutatua malalamiko yoyote yatakayojitokeza kwenye uchaguzi kwa kutumia njia za kisheria.

Na amerejea kusisitiza kuhusu nia ya Umoja wa Mataifa kuisaidia nchi hiyo katika juhudi za kuchagiza mshikamano wa kitaifa.

Kwa mujibu wa duru za Habari kuna wagombea 12 watakaochuana na Rais Alpha Conde mwenye umri wa miaka 82 kwenye uchaguzi huo utakaofanyika kesho tarehe 18 Oktoba.

Rais Conde anashiriki kinyan’ganyiro hicho akisaka awamu ya tatu ya uongozi iliyozua utata baada ya kufanya marekebisho ya katiba hali ambayo imezusha maandamano makubwa wiki hii la kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.