Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupitia mradi wa FAO sasa naweza kusomesha wanangu- Mnufaika Tanzania 

Baadhi ya wakulima wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa FAO, UNICEF na WFP nje ya ghala la kuhifadhi mpunga lililopo Kijiji cha Isele, Wilaya ya Iringa vijijini nchini Tanzania.
UN/Devotha Songorwa
Baadhi ya wakulima wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa FAO, UNICEF na WFP nje ya ghala la kuhifadhi mpunga lililopo Kijiji cha Isele, Wilaya ya Iringa vijijini nchini Tanzania.

Kupitia mradi wa FAO sasa naweza kusomesha wanangu- Mnufaika Tanzania 

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika kumulika wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutaka uwepo wa mifumo himilivu ya kilimo na inayohakikisha upatikanaji wa chakula  shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO nchini Tanzania linaendesha miradi kadhaa ya kilimo bora na uepushaji upotevu wa mazao kabla na baada ya kuvuna. 

Wanufaika ni pamoja na Idda Mtete, mkulima kutoka mkoani Iringa, ambaye anasema, “niko hapa ghala la Igodikafu ambalo tunahifaji mipunga yetu ikiwakilisha kata tatu. Mpaka dakika hii mimi ninanufaika na mradi huu kwa sababu nilishaanza kuwekeza gunia 30, nikakopesheka shilingi 200,000 nikapeleka mtoto ambaye ni yatima, mtoto wa mdogo wangu kwenda kusoma chuo Mwanza. Mwaka huu pamoja na mafuriko, nimebahatika kuleta magunia 45 ambazo ni nyongeza kwa magunia 15 na mpaka sasa nimekopa shilingi 350,000 ambazo nimeendelea kusaidia  watoto walioko chuo, mmoja yuko Tanga mwingine anaendelea Mwanza.” 

Bi. Mtete ambaye ni mjane anasema ingawa ana watoto watano, mradi huu naona nanufaika nao kwa sababu hata kukopesheka tunapata kirahisi kupitia stakabadhi benki mazao. Kwa kweli mradi huu una manufaa makubwa sana.” 

Mahamud Mwilwa ambaye pia ni mnufaika wa mradi wa FAO mkoani Iringa anatoa shukrani akisema, “FAO wametoa mafunzo ya kuweka mazao pamoja kwenye maghala na uendeshaji maghala na pia jinsi ya kupokea mazao yanayoingi akwenye maghala. FAO pia wametusaidia sana kwenye kilimo bora, mfano matumizi ya mbegu bora na pia vifaa vinavyokuwa rafiki kwa mkulima ili kuzuia upotevu wa mpunga. Wametupatia turubai na mizani ili kukabaliana na uhifadhi wa mazao ya mpunga.” 

Moja ya mashine za kukoboa mpunga katika mradi wa mpunga unaofadhiliwa na FAO,Kata Pagawa, Wilaya ya Iringa vijijini, Iringa, Tanzania.
UN/Devotha Songorwa
Moja ya mashine za kukoboa mpunga katika mradi wa mpunga unaofadhiliwa na FAO,Kata Pagawa, Wilaya ya Iringa vijijini, Iringa, Tanzania.

 

Pamoja na shukrani, Bwana Mwilwa ana ombi akisema, “hata hivyo bado tuna mahitaji  ambayo tunatarajia mradi utusaidie sisi wakulima. Tulipo hapa tunategemea mashine ya kukoboa iliyoko zaidi ya umbali wa kilometa 15. Hivyo tunaamini wazi baada ya kuwa ghala limekamilika, watusaidie hata tupate mashine ya kukoboa hapa jirani. Sisi tunachohitaji tuuze mchele na siyo mpunga.” 

Lakini janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limekuwa na athari gani katika utekelezaji wa miradi? , Charles Tulahi ni Mwakilishi Msaidizi wa FAO Tanzania upande wa miradi anafunguka akisema, “kwa kweli Corona imeathiri kwa kiasi fulani. Mathalani kuna maeneo ambako ilikuwa tujenge uwezo kwa kufanya mafunzo. Kwa kipindi fulani hatukuweza kufanya mafunzo kwa wakati, kwa hiyo hatukuweza kutekeleza kwa wakati kama ilivyokuwa kwa kuzingatia kuwa miradi mingine inakwenda na misimu ya kilimo, kwa hiyo inapofika kwamba uliowalenga hukuwafikia kwa wakati, inakuwa kwamba kilimo kinaweza kuathirika kwa namba mbalimbali.” 

Ingawa hivoy amesema pamoja na changamoto hizo, wameweza kutekeleza miradikwa kadri walivyoweza na kwamba, “tumechukulia kuwa ni changamoto na tumeweza kujifunza ili tuweze kujenga mifumo himilivu ambayo inaweza kuhimili mitikisiko yoyote kama Corona au inayoweza kujitokeza siku za usoni.”