Uhaba wa watu kunawa mikono kwa sabuni unawaweka mamilioni kwenye hatari kubwa zaidi

15 Oktoba 2020

Ingawa kunawa mikono kwa sabuni ni muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo COVID-19, mamilioni ya watu duniani hawana mahali pa kunawia mikono, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika siku ya kimataifa ya kunawa mikono hii leo.

 

Kelly Ann Naylor, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Maji, Kujisafi na Usafi wa UNICEF amenukuliwa akisema, “janga la COVID-19 limeangazia jukumu muhimu la usafi wa mikono katika kuzuia magonjwa. COVID-19 imesisitiza pia shida iliyopo kwa wengi: Kunawa mikono na sabuni hakuwafikii mamilioni ya watoto katika mazingira wanamozaliwa, kuishi na kujifunzia. Haikubaliki kwamba jamii zilizo katika mazingira magumu zaidi haziwezi kutumia njia rahisi kujilinda wao na wapendwa wao. Lazima tuchukue hatua za haraka ili kufanya kunawa mikono na sabuni vipatikane kwa kila mtu, kila mahali - sasa na baadaye. ” 

UNICEF inasema kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni, watu 3 pekee kati ya watu 5 ulimwenguni  kote ndio wana vifaa vya msingi vya kunawa mikono.  

Asilimia 40 ya watu wote duniani au watu bilioni 3, hawana vifaa vya kunawa mikono vyenye maji na sabuni nyumbani mwao. 

Takribani robo tatu ya watu katika nchi maskini zinakosa vifaa vya kunawa mikono nyumbani.  

Asilimia 43 ya shule hazina vifaa vya kunawa mikono vyenye maji na sabuni na hivyo kuwaathiri watoto milioni 818.  

Makadirio yameendelea kuweka wazi kuwa katika nchi maskini, shule 7 kati ya shule 10 hazina mahali pa watoto kunawa mikono kwa maji na sabuni.   

Aidha katika nchi 60 ambazo zimetambuliwa kama zenye hatari zaidi ya kiafya na majanga ya kibinadamu kutokana na virusi vya corona, watu 2 kati ya 3 yaani watu bilioni 1 kwa ujumla wanakosa  vifaa vya msingi vya kunawa mikono kwa sabuni na maji nyumbani na nusu ya watu wote hao ni watoto.  

Watoto 3 kati ya 4 wakati wa utafiti walionesha kukosa huduma za msingi za kunawa mikono katika shule zao mwanzoni mwa mlipuko wa janga la virusi vya corona, nusu ya watoto wote walikosa huduma za msingi za maji na zaidi ya nusu walikosa huduma za kujisafi.  

Vilevile kwa mujibu wa UNICEF, katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika, asilimia 63 ya watu katika maeneo ya mijini sawa na watu milioni 258 wanakosa mazingira ya kunawa mikono. Takribani asilimia 47 ya watu  wa Afrika Kusini kwa mfano, au watu milioni 18, wanakosa vifaa vya msingi vya kunawa mikono nyumbani.  

Mwanamke huko Gujarat, India, anaelimishwa juu ya faida za kunawa mikono wakati wa janga la COVID-19.
© UNICEF/Vinay Panjwani
Mwanamke huko Gujarat, India, anaelimishwa juu ya faida za kunawa mikono wakati wa janga la COVID-19.

 

"Katika Asia ya Kati na Kusini, asilimia 22 ya watu katika maeneo ya mijini, au watu milioni 153, wanakosa ufikiaji wa kunawa mikono. Karibu asilimia 50 ya watu wa mjini Bangladesh, kwa mfano, au watu milioni 29; na asilimia 20 ya Wahindi wa mijini, au watu milioni 91, wanakosa vifaa vya msingi vya kunawa mikono nyumbani." Inaeleza taarifa ya UNICEF. 

Katika Asia ya Mashariki, asilimia 28 ya Waindonesia wa mijini, au watu milioni 41, na asilimia 15 ya Wafilipino wa mijini, au watu milioni 7, hawana vifaa vya msingi vya kunawa mikono nyumbani. 

UNICEF inafanya kazi ulimwenguni kote kuhakikisha watoto na familia wanapata vifaa mwafaka vya kunawa mikono. Mbali na kuhamasisha unawaji mikono katika nchi zaidi ya 130, UNICEF na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO ilizindua mpango wa usafi wa mikono kwa wote kusaidia maendeleo ya mpango wa kitaifa ili kuharakisha na kudumisha maendeleo kuelekea kufanya usafi wa mikono kuwa tegemeo katika kushughulikia afya ya umma. Hii inamaanisha kuboresha haraka upatikanaji wa vifaa vya kunawa mikono, maji, sabuni na usafi wa mikono katika mipangilio yote, na pia kukuza hatua za mabadiliko ya tabia kwa mazoea ya usafi wa mikono. Kuwaleta pamoja washirika wa kimataifa, kitaifa, na wenyeji, mpango huo unakusudia kuhakikisha bidhaa na huduma zinazopatikana kwa bei nafuu na endelevu, haswa katika jamii zilizo katika mazingira magumu na hatarishi.  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter