Benki ya vijijini ni jawabu kwa wanawake wa vijijini wakati wa COVID-19 

Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
UN Women/Joe Saade
Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.

Benki ya vijijini ni jawabu kwa wanawake wa vijijini wakati wa COVID-19 

Wanawake

Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake wa vijijini ikimulika umuhimu wa kujenga mnepo kwa kundi hilo wakati huu ambapo dunia imekumbwa na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19. 

Umoja wa Mataifa kupitia ukurasa wake maalum wa siku hii, unasema kuwa “wanawake na wasichana wako upande wa changamoto zaidi wakati huu wa janga, changamoto ambayo inaongezwa zaidi ukizingatia mazingira wanamoishi ya vijijini. Wanawake wa vijijini, wakiwa na jukumu la msingi kwenye kilimo, uhakika wa chakula na lishe, wanakabiliwa na changamoto katika maisha yao ya kila siku.” 

Kwa sasa, tangu kuanza kwa janga la COVID-19 na mahitaji yao ya kipekee ya kiafya huko maeneo ya ndani zaidi, wako na fursa finyu zaidi kupata huduma bora za afya, matibabu na chanjo. Changamoto nyingine ni kukosa taarifa, teknolojia za kisasa kuboresha kazi zao na maisha yao sambamba na kuendelea na jukumu kubwa la malezi bila ujira wowote. 

Programu zilizofadhiliwa na IFAD ziliwapa mafunzo tofauti  wanawake zaidi ya milioni moja wa vijijini katika jimbo la Maharashtra India.
screengrab/IFAD
Programu zilizofadhiliwa na IFAD ziliwapa mafunzo tofauti wanawake zaidi ya milioni moja wa vijijini katika jimbo la Maharashtra India.

Ni kwa kuzingatia hilo, Umoja wa Mataifa unataka uwekezaji maeneo ya vijijini unaojali jinsia na ndio maana maudhui ya siku ya leo mwaka huu ni Kujenga mnepo wa wanawake wa vijiini wakati huu wa janga la COVID-19 na kuhamasisha juu ya machungu ya wanawake, mahitaji yao na dhima muhimu na ya msingi wanayobeba katika jamii. 

Nchini Sierra Leone, kwa msaada wa mfuko wa maendeleo ya kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD, mwaka 2013,  mwaka mmoja kabla ya Ebola kutikisa taifa hilo, ilianziishwa  benki za vijijini ambazo ziliwezesha wakulima wadogo kuendelea kupata mikopo. Benki hizo zilikuwa wazi na wakulima wanawake kwa wanaume waliweza kukopa fedha wakati wa janga hilo, baada na hata sasa wakati wa janga la COVID-19. 

Akikumbuka hali ilivyokuwa wakati wa Ebola, Zainab Kargbo ambaye ni mchuuzi anasema, “wakati wa Ebola nilikuwa najificha siku nzima na kurejea usiku. Ilikuwa vigumu kwetu, ulikuwa huoni wafanyabiashara na kulikuwa hakuna cha kuuza. Hakuna mfanyabiashara ambaye aliweza kutuuzia kitu na sisi hatukuweza kwenda kwao kununua chochote. Tulibakia msituni. Kwa hiyo maisha yalikuwa magumu sana kwetu. Magumu sana wakati wa Ebola.” 

Benki ya jamii iliyoanzishwa na IFAD ikageuka mkombozi kwa kaya zaidi ya 200,000 wakati wa Ebola na hata wakati wa sasa wa janga la COVID-19 kwa kuwa uwezo wao wa kukopa fedha umesaidia kuendeleza biashara zao. 

Bi. Kargbo anasema, “kwa mkopo wa dola 50, ninapatiwa kipindi cha miezi 6 kurejesha mkopo. Natumia fedha kukodisha trekta kwa ajili ya kupalilia shamba. Na fedha inayobakia nalipia karo ya shule watoto wangu. Unajua nina watoto wengi wanaokwenda shule.” 

Sharon Kirui, mkulima kutoka Kenya ambaye amenufaika na mradi wa IFAD na Muungano wa Ulaya kwa wakulima wadogowadogo.
IFAD/ Video
Sharon Kirui, mkulima kutoka Kenya ambaye amenufaika na mradi wa IFAD na Muungano wa Ulaya kwa wakulima wadogowadogo.

Guterres naye apaza sauti

Kwa kutambua changamoto za wanawake wa vijijini ambazo zinaongezeka zaidi hivi sasa wakati wa COVID-19, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii  amesema, “kwa pamoja ni lazima tuwekeze kwa wanawake wa vijijini ili wawe na fursa ya huduma ya afya, ulinzi wa kijamii na taarifa kuhusu kilimo. Lazima tupunguze pengo la teknolojia na kuwapatia huduma muhimu ili wakabiliane na kivuli cha janga la ukatili dhidi ya wanawake. Pia tuondoe sheria za kibaguzi za umiliki wa ardhi na urithi na mambo yanayofanya wanawake wa vijijini kuwa hatarini zaidi kupoteza vipato vyao.”

Katibu Mkuu amesema katika siku ya leo hebu kila mtu arejelee ahadi yake kwa wanawake wa vijijini kwa kutambua  utofauti wao, “kuongeza jitihada zetu za kuwasaidia wakati huu wa janga la Corona na kufanya nao kazi ili kujenga mnepo dhidi ya majanga yajayo.”

 

Je wajua?

Wanawake wa vijijini – robo ya idadi ya watu wote duniani – wanafanya kazi ya kilimo, wanapata kipato na ni wajasiriamali.

Nusu ya asilimia 20 ya wamiliki wa ardhi duniani ni wanawake. Katika maeneo ya vijijini, pengo la ujira kijinsia kati ya mwanamke na mwanaume ni asilimia 40.

Kwa kupunguza kiwango cha pengo la ujira duniani kwa asilimia 25 kati ya mwanamke na mwanaume, kunaweza kuongeza pato la ndani la taifa kwa asilimia 3.9 ifikapo mwaka 2025.

Iwapo wanawake wa vijijini wanapata sawa na wanaume pembejeo za kilimo, elimu na masoko, uzalishaji kwenye sekta ya kilimo unaweza kuongezeka na idadi ya watu wenye duniani inaweza kupungua kwa kati ya milioni 100 hadi milioni 150.