Miaka 3 baada ya shambulio la kigaidi Moghadishu UN yashikamana na Wasomali:UNSOM 

14 Oktoba 2020

Leo ni kumbukumbu ya miaka mitatu tangu kufanyika kwa shambulio kubwa zaidi la kigaidi mjini Moghadishu Somalia mnamo 14 Oktoba 2017. 

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM leo umeungana na wananchi wa Taifa hilo la Pembe ya Afrika kuwaenzi waathirika na manusura wa shambulio hilo la kikatili na kusisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kushikamana na Wasomali wote. 

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa mwakilishi maalum wa Umoja huo nchini Somalia na mkuu wa UNSOM James Swan amesema “ Kwa pamoja na Wasomali, familia ya Umoja wa Mataifa inajikita na mustakabali wa taifa hili na kuendelea kusongesha mchakato wa kuelekea amani, utawala bora na mfanikio. Hatua zilizopigwa tangu 2017 ni dhihirisho la mnepo wa Wasomali na dhamira ya kuwa na mustakabali bora kesho licha ya machafuko na ukatili wa itikadi kali.” 

Bwana Swan amesisitiza kuwa “Ukatili wa shambulio la 14 Oktoba 2017 hautosahaulika asilani, na fikra na mawazo yetu yanaendelea kuwa na familia za wale waliopoteza maisha na manusura.” 

Shambulio hilo lililokatilio Maisha ya watu 587 na kujetuhi wengine wengi limetajwa kuwa ndio shambulio baya zaidi  la kigaidi barani Afrika la kutumia vifaa vya mlipuko (IEDs). 

Shambulio hilo linaloshukiwa kufanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab lilitokea katikati ya mji wa mkuu Moghadishu baada ya lori lililokuwa limesheheni mamia ya kilo za vilipuzi na mabomu ya kutengenezwa nyumbani kulipuka kwenye eneo la mkusanyiko wa watu wengi. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud