Wakimbizi wa Kisomali waungana kusaidia wenyeji wao, wahamiaji na wasaka hifadhi Afrika Kusini. 

14 Oktoba 2020

Nchini Afrika Kusini, jamii ya wakimbizi wa Kisomali wameamua kushirikiana na majirani zao raia wa Afrika Kusini kuwasaidia watu ambao wanahangaika na maisha katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 nchini humo.

Jumuiya ya wafanyabiashara wa kisomali wameanzisha kampeni hiyo ya kusaidia watu wenye mahitaji makubwa ya msingi tangu Afrika Kusini ilipofunga mipaka mwezi Machi mwaka huu kutokana na janga la COVID-19. Walianza kwa kusambaza barakoa, vitakasa mikono na vifurushi vya chakula katika makazi yasiyo rasmi mjini Pretoria na Johannesburg kisha wakahamia katika maeneo mengine ya nchi.   

Saeed Mohamed, mkimbizi wa Kisomali aliyekimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe Somalia mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 17, yuko katika kitovu cha msaada huu akikumbuka ukarimu aliofanyiwa alipokimbilia Afrika Kusini na baadaye akafanikiwa kusoma hadi kufikia katika kazi ya benki. Virusi vya corona vimempa fursa ya kurejesha fadhila, anasema,“unajua nini, hapa kuna watu waliotukaribisha katika nchi yao na ambao ni wenyeji wetu katika nchi yao.”  

Serikali ya Afrika Kusini inatoa msaada kwa maelfu ya watu na biashara lakini makundi kama wasaka hifadhi, wakimbizi wasio na nyaraka za kutosha, wahamiaji wasi wa kawaida na wasio na makazi, hawako katika mpango wa msaada wa serikali. Regina ni raia wa Afrika Kusini, mmoja wa wanaopokea msaada kutoka kwa wakimbizi wa Kisomali, "Tunahangaika kununua chakula na zaidi pesa tunazopata hazitoshelezi gharama zote tulizonazo nyumbani.”  

Désirée Boyseen, ni mmoja wa Raia wa Afrika Kusini kutoka eneo la Port Elizabeth ambaye anasaidiana na wageni kusambaza msaada na anaonekana kakiwa katika shughuli ya kugawa chakula  kwa raia wa Afrika Kusini wasio na makazi, wahamiaji na wasaka hifadhi, wengi wao wakiwa wamepoteza kazi, anasema, “sichagui kabisa mtu wa kumsaidia. Ninapokutana na wahitaji, ninaona watu ambao wanahitaji, ninawasiliana nao.” 

Afrika Kusini ni mwenyeji wa takribani wakimbizi 266,700 na wasaka hifadhi. Takriban asilimia 30 ni kutoka Somalia, asilimia 29 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na asilimia 20 kutoka Ethiopia, na waliosalia wengi wao wakiwa kutoka Zimbabwe na Jamhuri ya Kongo. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter