UNDP yaleta matumaini kwa wakulima wa Habanero nchini Tanzania

Nchini Tanzania, shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP limewezesha chama cha wakulima wa mboga na matunda nchini humo, TAHA kusaidia wanachama wake kulima kilimo bora cha mazao hayo kupitia mashamba ya mfano na ya kisasa na sasa wanapata masoko nchi za nje.
Ujumbe wa UNDP uliotembelea mashamba ya TAHA mkoani Kilimanjaro na Arusha ulishuhudia mashamba yakiwa yameshamiri na wakulima wakiwa na matumaini siyo tu ya kuvuna mazao bora bali pia kupanua kilimo chao.
Miongoni mwa wanufaika ni Betty Gadson Mrema wa kikundi cha Umwagiliaji Uchira kinachomiliki shamba la mfano la Pilipili aina ya Habanero kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.
Bi. Mrema anasema, “kikundi chetu kina wanachama 30 na tuliamua kuunda kikundi kwa kuwa ukiwa na kikundi kuna faida nyingi kama vile mnapata watu wa kuwaelekeza, maafisa ugani wanakuwa karibu na sisi, tunapata elimu, wanatufundisha. Pia wametueleza watatupatia wafadhili na udhamini.”
Alipoulizwa ni kwa nini waliamua kulima pilipili na si kilimo kingine, mwanachama huyo wa kikundi cha Umwagiliaji Uchira kinachoratibiwa na TAHA amesema, “tuliamua kulima pilipili kwa sababu tuliona ni klimo kizuri na kina soko, tuliambiwa soko lake liko nje kwa hiyo kinakuwa ni cha uhakika. Hii ni tofauti na kilimo kingine ambacho tulikuwa tunalima. Tulikuwa tunalima na mazao na yanabakia shambani na hakuna mtu wa kununua.”
Kwa kikundi hiki, kilimo cha sasa cha pilipili aina ya Habanero ni cha kwanza, lakini awali walilima la uhakika. Hii ni tofauti na kilimo cha mazao mengine kama nyanya, vitunguu na pilipili mbuzi ambazo wameshavuna na kwamba, “sasa tumeingia kwenye kilimo hiki tulichoambiwa ni cha mkataba na kina faida kwa sababu tayari tuna mahali pa kuuza, tofauti na kile cha kwanza ambacho kilikuwa ni cha kutafuta soko, kwa hiyo hatukupata faida kulingana na masoko. Sasa tuna uhakika kuwa tukivuna pilipili tuna mahali pa kupeleka.”
Enock Florian Ngowi ni bwana shamba wa TAHA mkoani Kilimanjaro ambaye anasema kuwa walichagua eneo lenye joto katika kijiji cha Kyomu Kata ya Kahe kwa kuwa hali hiyo ya hewa ni murua kwa kilimo cha pilipili aina ya Habanero.
“Pilipili zinakomaa baada ya miezi miwili na nusu tangu kuhamishiwa shambani kutoka kwenye kitalu. Na unaweza kuvuna kwa muda mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu. Na kila wiki unaweza kuvuna pilipili,” amesema Bwana Ngowi.
UNDP Tanzania inatekeleza mradi huo wa kilimo endelevu ikilenga vijana na wanawake.
Maeneo ambayo tayari yananufaika ni Arumeru mkoani Arusha, Moshi vijijini, Siha na Same mkoani Kilimanjaro, Bunda mkoani Mara, Busega mkoani Simiyu na wilaya za Njombe, Wanging’ombe na Ludewa mkoani Njombe.
Kwa sasa TAHA kupitia msaada wa UNDP inajenga vituo vinne huko Same mkoani Kilimanjaro.