Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike: Fursa ya kuunda ulimwengu bora, mzuri na sawa kwa wasichana kila mahali. 

Wasichana wadogo wakiwa darasani nchini Sri Lanka
World Bank/Deshan Tennekoon
Wasichana wadogo wakiwa darasani nchini Sri Lanka

Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike: Fursa ya kuunda ulimwengu bora, mzuri na sawa kwa wasichana kila mahali. 

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya mtoto wa kike anasema wasichana barubaru, na harakati za ulimwengu za mabadiliko wanazounda, ndio viongozi wapya wa wakati wetu.

Bwana Guterres kupitia ujumbe huo anasisitiza, “wacha tujitahidi kukuza vipaji vyao na kupaza sauti zao, na tufanye kazi pamoja kwa maisha bora ya baadaye na yaliyo sawa kwa sisi sote.” 

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Sauti Yangu: Mstakabali wetu ulio sawa," na Katibu Mkuu Guterres anasema kwamba hii inatuhimiza kupaza sauti ya wasichana barubaru na kuweka mahitaji yao mbele wakati wa kuandaa sheria, sera na utekelezaji katika kila nchi na jamii kote ulimwenguni. 

Ulimwenguni, idadi ya wanawake kati ya wahitimu wa masomo ya sayansi, ni chini ya asilimia 15 katika zaidi ya theluthi mbili ya nchi, kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye anasisitiza kuwa, "hali haipaswi kuwa hivyo." 

Amina Muhammad: Kuweni na ujasiri katika madai yako 

Siku ya Ijumaa, Umoja wa Mataifa uliandaa mjadala wa wazi kupitia mtandao wa intaneti ili kusherehekea siku hii ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, na tukio hilo lilishirikisha wanaharakati wachanga kutoka kote ulimwenguni. 

Wakati janga la COVID-19 linapoongeza ukosefu wa usawa wa kijinsia na uchumi, washiriki walidai ulimwengu wa haki na usawa zaidi kwa wasichana. 

Viongozi na watunga sera walizungumza kuhusu  masuala muhimu kwa ajili ya kulinda na kuwawezesha wasichana wadogo. Katika hotuba yake ya ufunguzi katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Amina Mohamed, akiwahutubia wasichana hao, aliwaambia, “kuwa na ujasiri katika madai yanu na ujasiri katika kila hatua mtakayochukua. "