Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yashinda tuzo ya amani ya Nobel 2020

Helikopta ya WFP ikisambaza chakula
UNICEF/Peter Martell
Helikopta ya WFP ikisambaza chakula

WFP yashinda tuzo ya amani ya Nobel 2020

Masuala ya UM

Kamati ya tuzo ya amani ya Nobel yenye makao yake nchini Norway leo imelitangaza shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP kuwa ndio mshini wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huuu wa 2020. 

Ikitangaza tuzo hiyo kamati imesema “ni kwa sababu ya mchango mkubwa wa WFP katika kupambana na njaa, kwa mchango wake wa kuleta mazingira ya amani katika maeneo yenye migogoro na kwa kuwa chachu ya juhudi za kuzuia njaa kutumika kama silaha ya vita na migogoro.” 

Tweet URL

 

Kwa upande wake WFP ikishukuru kwa tuzo hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema “Hii ni kutambua kazi kubwa ya wafanyakazi wa WFP ambao wanaweka Maisha yao hatarini kila siku ili kufikisha chakula na msaada kwa zaidi ya watu milioni 100 wenye njaa wakiwemo Watoto, wanawake na wanaume kote duniani.” 

Akiipongeza WFP kwa ushindi huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Nimefurahi kwa uamuzi wa kamati ya tuzo ya amani ya Nobel kulitunukia shirika la Umoja wa Mataifa la WFP tuzo ya amani yam waka huu. WFP ndilo shirika la kwanza duniani kuwa msitari wa mbele kukabiliana na kutokuwa na uhakika wa chakula. Waume na wanawake wa WFP wanawanapitia hatari na safari ndefu kufikisha msaada wa kuokoa Maisha kwa wale walioathirika na migogoro, kwa watu wanaotaabika sababu ya majanga, kwa Watoto na familia wasio na uhakika mlo wao unaofuta unatoka wapi.” 

Guterres ameongeza kuwa katika dunia iliyosheheni inasikitisha kwamba mamilioni ya watu wanalala njaa na mamilioni wengine wako katika hatihati ya baa la njaa kutokana na janga la corona au COVID-19

Amesema hivi sasa dunia inakabiliwa pia na njaa ya ushirikiano wa kimataifa na WFP inalisha njaa hiyo pia, shirika hilo linafanyakazi kubwa zaidi ya kivuli cha kisiasa katika operesheni za kushughulikia mahitaji ya kibinadamu na shirika hilo linatekeleza majukumu yake kwa kutegemea michango kuytoka nchi wanachama kwa kiasi kikubwa na pia kutoka kwa umma. 

Amesisitiza kwamba mshikamano huo unahitajika sasa kushughulikia sio tu janga la COVID-19 lakini changamoto zingine za kimataifa katika zama hizi. 

Hivyo Guterres amesema, “nampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley na wafanyakazi wote wa WFP kwa kuendeleza maadili ya Umoja wa Mataifa kila siku na kutimiza matakwa ya sisi watu , wakati shirika hili likiadhimisha miaka 75.” 

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (wa pili kulia) na David Beasley(kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP wakigawa chakula kwa wakimbizi wapya kwenye makazi ya Imvepi nchini Uganda.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (wa pili kulia) na David Beasley(kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP wakigawa chakula kwa wakimbizi wapya kwenye makazi ya Imvepi nchini Uganda.

Pongezi zaidi kutoka ndani ya UN

Wakati huo huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ametuma salamu zake za dhati kwa WFP akielezea mchango wake wa thamani kama mhimili mkuu wa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa unaosaidia uhai wa mamilioni ya watu walio hatarini zaidi na kwamba ni WFP imestahili kupata tuzo hiyo ya amani ya Nobel.
“Pamoja na kutoa msaada wa chakula kwa takribani mataifa 90, WFP ni mdau muhimu katika kupambana na COVID-19, kusafirisha wahudumu wa misaada na misaada ya kibinadamu, na kusaidia upatikanaji na usambaaji wa bidhaa hizo muhimu kama vile vifaa vya kujikinga, PPE na vile vya kusaidia kupumua,”  amesema Bozkir.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, Munir Akram, ametoa pongezi kwa WFP kupitia mtandao wake wa Twitter akisema “katikati ya janga la COVID-19, mmeendelea kuimarisha juhudi zenu kufikishia misaada wale walio hatarini zaidi. Ni mafanikio yaliyostahili kabisa.”