COVID-19 yaongezea wazee jukumu la kulea wajukuu

9 Oktoba 2020

Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 limefichua siyo tu hatari zinazowakumba wazee bali pia mchango wao adhimu katika kulea wajukuu zao. Hivyo ndivyo kwa Ruth Sandrum kutoka Malawi ambaye yeye anajivunia kuwa mlezi wa wajukuu zake.

Kijiji cha Kasale nchini Malawi kutana na Ruth Sandrum, ambaye anasema anajisikia vizuri sana kuwepo na mjukuu wake wa kiume aitwaye Yotamu Stanford. Anasema Yotamu, si mjukuu wa kwanza wa kiume kumlea bali ni wa tatu.

Bi. Ruth anayeishi na binti yake na wajukuu watano, anasema ndoto yake ni kumuona Yotamu mwenye umri wa miaka 14 anajiunga na masomo ya sekondari na huo utakuwa urithi bora zaidi ambapo Yotamu anasema, “ananitia moyo kwenye masomo yangu, na anasisitiza niende shule ili niwe na maisha mazuri nikimaliza masomo nataka kuwa daktari.” 

Katika nchi za kusini mwa Afrika, babu na bibi wamekuwa wakichukua hatua zaidi kuhakikisha ustawi wa wajukuu zao na sasa wakati wa janga la COVID-19 wamegeuka kuwa walezi licha ya wao pia kuwa katika hatari kubwa kuambukizwa ugonjwa huo.

© UNICEF/Benny Khanyizira
Ruth Sandrum mwenye umri wa miaka 71, ambaye ni mjane na mama wa watoto 5 na wajukuu 13 akichambua kuni nje ya makazi yao huko Kasale, wilaya ya Ntcheu nchini Malawi.

Ili kujipatia kipato na kuweza kulea wajuu, Bi. Ruth hulima mahindi na maharagwe kwa kuwa,“maisha yana changamoto nyingi. Changamoto kubwa kwangu ni ukosefu wa chakula. Gonjwa la Corona limeniathiri sana. Ni ugonjwa mbayá sana. "

Serikali ya Malawi imesikia kilio chao na kwa msaada wa UNICEF kupitia mpango wa kunusuru kaya kijamii uitwayo Mtukula Pakhomo, katika miezi mitatu familia yao imepatiwa dola 7 sawa na Kwacha za kimalawi 6,500.

Kitendo hicho kinatoa kauli kwa Ruth akisema, “nashukuru sana kwa msaada huo wa fedha. Kaya yetu sasa imebadilika, naweza kununua chakula kwa ajili ya wanangu. Ninapopokea hiyo fedha naiweka katika kikundi cha kijiji cha akiba na mkopo ili iweze kuongezeka. “

Mwaka 2020, takribani kaya 291,322 zilipata msaada huo wa fedha ambapo kati yao hizo, 134,593 zinaongozwa na wazee kama Bi. Ruth.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter