Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yanayoendelea Sudan ni janga juu ya janga:FAO 

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP linasema hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kwa kazi wakati mwimbi la njaa likienea katika nchi ambayo ina mgogoro, mvua kubwa na mafuriko.
Image captured from a WFP video
Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP linasema hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kwa kazi wakati mwimbi la njaa likienea katika nchi ambayo ina mgogoro, mvua kubwa na mafuriko.

Mafuriko yanayoendelea Sudan ni janga juu ya janga:FAO 

Tabianchi na mazingira

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema mafuriko yanayoendelea katika majimbo 17 kati ya 18 ya nchini Sudan ni janga juu ya janga na kuichagiza jumuiya ya kimataifa kupeleka msaada wa haraka kunusuru maisha ya maelfu ya watu.  

Kwa mujibu wa Dominique Burgeon mkurugenzi wa FAO idara ya masuala ya dharura na msaada aliyekwenda kutathimini hali halisi ya athari za mafuriko hayo kwa mustakbali wa chakula nchini humo, hali ni mbaya na kinachohitajika hivi sasa ni fedha za kuisaidia Sudan ambayo tayari ilikuwa na kiwango kikubwa cha njaa na kutokuwa na uhakika wa chakula hata kabla ya mafuriko na janga la corona au COVID-19 kuzuka.“Mafuriko haya ni mabaya sana na makubwa kuwahi kuiathiri nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 70. Tumefanya tathimini ya haraka na wizara ya kilimo ya Sudan na kubaini kwamba zaidi ya kaya laki sita zimeathirika na mafuriko haya, na zaidi ya ekari milioni 2.2 zimesambaratishwa, kwa hiyo hali ni mbaya sana.” 

Ameongeza kuwa na kibaya zaidi mafuriko haya yamekuja wakati taifa hilo likielekea msimu wa mavuno na hivyo kuharibu mazao yaliyokuwa tayari na kuzidisha hofu ya njaa ukizingatia kwamba tayari  hali ilikuwa mbaya kwa mamilioni ya watu waliopoteza pia mifugo, nyumba zao na wengine kila kitu.

Kabla ya mafuriko FAO inasema watu milioni 9.6 Sudan walikuwa katika kiwango cha juu cha kutokuwa na uhakika wa chakula na sasa ukichanganya matatizo mengine kama nzige, machafuko katika baadhi ya maeneo na COVID-19, taifa hilo na watu wake wako njiapanda na asilimia kubwa wanalazimika kushinda njaa “Hii inamaanisha wanapunguza kiwango na idadi ya milo, na tulichobaini ni kwamba katika wakati huu tayari walikuwa wanakula mlo mmoja tu kwa siku, hivyo hali ni mbaya sana na watu hawa wanahitaji haraka msaada wetu.” 

FAO imeonya kwamba endapo msaada wa fedha za kukabiliana na hali ya sasa hautopatikana haraka, basi jumuiya ya kimataifa ijiandae kwa janga kubwa litakalohitaji mshikamano wa mashirika kupeleka msaada wa dharura kuepusha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.