Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila sekunde 16 mtoto 1 duniani huzaliwa mfu- Ripoti 

Mwanamke ambaye mtoto wake alizaliwa mfu baada ya uchungu wa zaidi ya saa 10, akiwa amelala kwenye wodi ya wazazi nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Olivier Asselin
Mwanamke ambaye mtoto wake alizaliwa mfu baada ya uchungu wa zaidi ya saa 10, akiwa amelala kwenye wodi ya wazazi nchini Sierra Leone.

Kila sekunde 16 mtoto 1 duniani huzaliwa mfu- Ripoti 

Afya

Katika kila sekunde 16 mtoto mmoja huzaliwa mfu, imesema ripoti mpya ya aina yake iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake, idadi ambayo ni sawa na watoto milioni 2 kila mwaka. 

Mashirika hayo lile la afya, WHO, la kuhudumia watoto, UNICEF, Benki ya Dunia na Idara ya Uchumi na kijamii ya UN, DESA wametoa ripoti hiyo leo Geneva Uswisi na New York, Marekani ikipatiwa jina Janga lililopuuzwa:Mzigo wa dunia wa watoto wanaozaliwa wafu. 

 Idadi kubwa ya vifo hivyo, sawa na asilimia 84 ni katika nchi za kipato cha chini na kati, ambapo kwa takwimu hizo za mwaka 2019, vifo vitatu kati ya vinne ni katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. 

Ripoti imeainisha mtoto mfu ni yule anayefia tumboni au wakati anazaliwa bila kuwa na dalili zozote za uhai kuanzia wiki 28 za ujauzito na kuendelea. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19, linaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi, “kupungua kwa huduma za afya kwa asilimia 50 kutokana na Corona kunaweza kusababisha watoto takribani 200,000 kuzaliwa wafu katika nchi 117 za kipato cha chini na kati.” 

Baada ya mtoto wake kuzaliwa mfu, mama huyu amerejea nyumbani na anapakua kutoka kwenye mfuko wake nguo na blanketi za mtoto nyumbani kwake Lusaka, Zambia.
©UNICEF/Nesbitt
Baada ya mtoto wake kuzaliwa mfu, mama huyu amerejea nyumbani na anapakua kutoka kwenye mfuko wake nguo na blanketi za mtoto nyumbani kwake Lusaka, Zambia.

Je wafahamu sababu za watoto kuzaliwa wafu?

Sababu za kuwepo vifo hivyo zimetajwa kuwa ni huduma duni wakati wa ujauzito na kujifungua. Ripoti inasema changamoto kubwa ni ukosefu wa uwekezaji katika huduma za kliniki kwa mama mjamzito na wakati wa kujifungua na uhaba wa wauguzi na wakunga. 

Ripoti inatanabaisha kuwa katika nchi za kipato cha chini na kati, hata kabla ya Corona, idadi ya wajawazito waliokuwa wanapata huduma bora ili kuepusha watoto kuzaliwa wafu ilikuwa ni ndogo. 

Nusu ya nchi 117 zilizoshiriki kwenye utafiti wa ripoti zilikuwa na kiwango cha chini ya asilimia 2 au haikuzidi asilimia 50 huduma muhimu 6 ambazo mjamzito atahitaji. 

Kadiatu Sama, ambaye hakupata huduma yoyote ile wakati wa ujauzito na ambaye mwanae alizaliwa mfu, akiwa anafarijiwa na muuguzi wa kike kwenye wodi ya wazazi ya hospitali ya serikali nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Pirozzi
Kadiatu Sama, ambaye hakupata huduma yoyote ile wakati wa ujauzito na ambaye mwanae alizaliwa mfu, akiwa anafarijiwa na muuguzi wa kike kwenye wodi ya wazazi ya hospitali ya serikali nchini Sierra Leone.

Huduma muhimu kwa mama mjamzito ili kuepusha uzazi mfu

Huduma hizo ni pamoja na kujifungua kwa upasuaji, kinga dhidi ya Malaria, udhibiti wa shinikizo la damu wakati wa ujauzito na uchunguzi na tiba dhidi ya kaswende. 

Kama hiyo haitoshi, ni nusu tu ya wanawake ambao wanahitaji huduma za kujifungua kwa njia ya kawaida waliweza kupata usaidizi unaotakiwa ili kuepusha mtoto kuzaliwa mfu. 

  Ni kwa mantiki hiyo ripoti inasema licha ya mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya watoto wachanga, uwekezaji wa  kuepusha mtoto kuzaliwa mfu  bado ni mdogo mno.

Kuzaa mtoto mfu ni pigo kubwa kwa mwanamke na familia

Akizungumzia takwimu hizo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Gebreyesus amesema “kukaribisha mtoto duniani ni kitu kinapaswa kuwa cha furaha, lakini kila uchao maelfu ya wazazi wanakumbwa na majonzi kwa sababu watoto wao wamezaliwa wafu. Janga hili linaonesha ni kwa  jinsi gani ni muhimu kuimarisha na kuendeleza huduma muhimu za afya sambamba na kuongeza idadi ya wauguzi na wakunga.” 

Kwa upande wake Henrietta Fore ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF“kupoteza mtoto wakati wa kujifungua au tumboni ni janga kubwa la kushtusha familia, janga ambalo huuguliwa kimya kimya licha ya kwamba limeenea duniani. Zaidi ya kupoteza mtoto, gharama za kisaikolojia na kifedha kwa wanawake, familia na jamii hudumu muda mrefu.“ 

Katika nchi tajiri nako tatizo hilo lipo, ambapo ripoti imesema ni kwa makabila madogo ikitolea mfano Canada “watu wa jamii ya Inuit wanakabiliwa sana na tatizo la kuzaa mtoto mfu mara tatu zaidi kuliko raia wa makabila mengine nchini humo. Na wanawake wamarekani weusi nchini Marekani hukumbwa na tatizo hilo mara mbili zaidi kuliko wamarekani weupe.” 

Ripoti inataka mwanamke yeyote mjamzito aendelee kupata huduma bora za afya wakati wote wa kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua ambapo Benki ya Dunia imesema inachofanya ni kuwezesha nchi kuimarisha mifumo yao ya afya ili kuzuia vifo hivyo na kuhakikisha wajawazito wanweza kupata huduma bora za afya.