Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa afya TANZBATT 7 wapatiwa mafunzo dhidi ya COVID-19

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.

Wataalamu wa afya TANZBATT 7 wapatiwa mafunzo dhidi ya COVID-19

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC shughuli za ulinzi wa amani zinazofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wa kikosi cha 7, TANZBATT 7 cha kikosi cha kujibu mashambulizi FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO zinaendelea sambamba na kuelimishana jinsi ya kujikinga na gonjwa la Corona au COVID-19 ambalo bado ni tisho duniani.Luteni  Issa Mwakalambo, Afisa Habari wa TANZBATT 7 amefutilia mafunzo hayo na kutuandalia taarifa hii kutoka Beni jimboni Kivu Kaskazini. 

Mafunzo hayo kwa wataalamu wa afya wa TANZBATT 7 yanalenga kuwajengea uwezo na matumizi sahihi ya vifaa hivyo na jinsi ya kuwahudumia wagonjwa iwapo watakuwa wameambukizwa. 

Pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yanakwenda sanjari na kufuata kwanini zote muhimu za afya kama vile kuna maji tiririka na sabuni wanapotoka na kuingia ndani ya eneo husika. 

Mganga Mkuu wa TANZBATT 7 Dkt. Meja Francis Ikea anaeleza matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga akisema, “unavaa kinga uso au miwani kama unazo, japo hapa hajavaa kofia ambayo unatakiwa uanze nayo. Kama hili gauni la kitabibu halina kofia inabidi uanze na kofia, lakini hii ina kikofia chake. Hii inasaidia hata ukiwa umeshavaa glovu zake isijetena ukaanza kutafuta kuvaa kofia.  Kwa hiyo inategema na PPE unayovaa. Ukishamaliza hapo ndio unavaa glovu. Sasa kwa kuwa sisi tunavaa glovu mbili, basi unaanza na moja halafu nyingine unavaa mwishoni. Ukishamaliza kuvaa gauni, unavaa barakoa.  

Mafunzo hayo ni kwa ajli ya askari na maafisa wanaotoa huduma za afya kwa wakazi wa Beni ambako ndiko kikundi cha TANZBATT 7 kimepiga kambi kusaidia kukabiliana na vikundi vilivyojihami kwenye eneo hilo. 

Tangu kubainika kwa Corona au COVID-19 mwezi Machi mwaka huu huko DRC, zaidi ya watu 10,000 wameugua COVID-19 na kati yao hao 274 wamefariki dunia. Hata hivyo idadi ya wagonjwa na vifo imeanza kupungua tangu mwezi uliopita wa Septemba na shule zimeanza kufunguliwa.