Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia haikuwa imejiandaa na janga la Corona, tumeumbuka- Guterres

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua wakati wa kampeni ya chanjo huko Impfondo, Jamhuri ya Congo
© UNICEF/Mariame Diefaga
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua wakati wa kampeni ya chanjo huko Impfondo, Jamhuri ya Congo

Dunia haikuwa imejiandaa na janga la Corona, tumeumbuka- Guterres

Afya

Miezi 9 tangu kusikia kwa mara ya kwanza kuhusu ugonjwa wa Corona au COVID-19, janga hilo tayari limeshasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni moja miongoni mwa zaidi ya watu milioni 30 waliothibitika kuwa na ugonjwa huo katika nchi 190.

Hivyo ndivyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwenye tamko lake la kisera lililotolewa leo jijini New York, Marekani lihusisha COVID-19 na huduma za afya kwa wote.

Guterres amesema maambukizi yanaongezeka na kuna viashiria vya kutia hofu kuhusu kuibuka kwa maambukizi mapya na kwamba bado virusi hivi havitambuliki ipasavyo lakini cha msingi ni kwamba dunia haikuwa imeajiandaa.

Muuguzi akiandaa chanjo katika kliniki moja huko Ramallah, Palestina
© UNICEF/Ahed Izhiman
Muuguzi akiandaa chanjo katika kliniki moja huko Ramallah, Palestina

Katibu Mkuu amesema, “janga limefichua ukosefu wa mifumo ya kutosha ya afya, pengo kwenye hifadhi ya jamii na ukosefu mkubwa wa usawa kati ya mataifa. Lazima hili liwe somo kwetu sote.”

Katibu Mkuu amesema fundisho kubwa ni kwamba uwekezaji dhaifu kwenye mifumo ya afya unaweza kuwa na madhara makubwa kwenye jamii na uchumi

Ametolea mfano hivi sasa ambapo COVID-19 inagharimu uchumi wa dunia dola bilioni 375 kila mwezi, ajira zipatazo milioni 500 zimetoweka hadi sasa na maendeleo ya binadamu yamepinduka, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kipimo cha maendeleo ya binadamu kianze kufanyika mwaka 1990.

Mifumo ya huduma ya afya ni dhaifu

Hata hivyo amesema kilichofichuliwa na COVID-19 ni umuhimu wa huduma ya afya kwa wote, mifumo thabiti ya afya kwa umma na kujiandaa kwa dharura yoyote kwa ajili ya kila jamii, kila uchumi na kila mtu.
Amesema hicho ndio msingi wa tamko lake la kisera analozindua leo wakati huu ambapo takribani nusu ya wakazi wa dunia hawana huduma za afya wanazohitaji. Watu milioni 100 wanatumbukia kwenye umaskini kila mwaka kutokana na gharama za matibabu.
Guterres amesema pengo hilo kwenye huduma ya afya ni sababu kwa nini COVID-19 imesababisha maumivu na machungu makubwa.

Janga limefichua ukosefu wa mifumo ya kutosha ya afya, pengo kwenye hifadhi ya jamii na ukosefu mkubwa wa usawa kati ya mataifa. Lazima hili liwe somo kwetu sote -  António Guterres, Katibu Mkuu wa UN

Nini kinahitajika kuimarisha huduma ya afya kwa wote?

“Huduma ya afya kwa wote, UHC, inahitaji serikali kuongeza uwekezaji wake kwenye afya, ikiwemo ufuatiliaji na mawasiliano ya kwenye hatari ili dunia isikumbwe ten ana janga kama la Corona,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika inahitaji miradi ya afya ya ymma ambayo ni jumuishi, yenye uwiano na isiwe na vikwazo vya kifedha, “huduma za afya hazipaswi kutegemea uwezo wa mtu kifedha.”

Amekumbusha kuwa mataifa yote yalikubaliana kuwa huduma ya afya kwa wote, UHC iwe sehemu ya ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Sampuli zikipimwa na wanasayansi katika Taasisi ya Jenner ya Chuo Kikuu cha Oxford ikiwa ni katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya virusi vya corona.
University of Oxford/John Cairns
Sampuli zikipimwa na wanasayansi katika Taasisi ya Jenner ya Chuo Kikuu cha Oxford ikiwa ni katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya virusi vya corona.


Mapendekezo matano

Hata hivyo amesema haiwezekani kusubiri miaka 10 ijayo, hivyo ametoa mapendekezo matano ya kutekeleza tamko lake la kisera.

Pendekezo la kwanza linahusu siyo tu huduma ya afya kwa wote bali pia afya ya akili na kuimarisha juhudi dhidi ya janga la Corona na kujiandaa kwa majanga yajayo.

Pili, udhibiti wa kuenea zaidi kwa COVID-19 kupitia mikakati iliyothibitishwa ya afya ya umma na hatua za kimataifa zilizoratibiwa.

Pendekezo la tatu ni kuendeleza huduma nyingine za afya wakati wa janga la Corona, “COVID-19 kwa njia nyingine inaua watu kupitia magonjwa ya moyo, saratani na wale wanaoambukizwa ugonjwa huo. Kupata huduma za afya ya akili, afya ya uzazi hakuwezi kusahaulika.”

Nne ni kuhakikisha kila mtu popote pale alipo anapata chanjo ya COVID-19 pindi itakapopatikana sambamba na tiba na uchunguzi. Amekumbusha kuwa kupatia fedha mfumo wa kuchagiza upatikanaji wa chanjo, ACT ndio njia pekee kumaliza janga la Corona.

Na mwisho ni kuimarisha uwezo wa kujiandaa kukabili janga akisema “hii inamaanisha kujumuisha sekta zote na kuwekeza katika mifumo ya kutoa hadhari itakayowezesha mamlaka za afya kuchukua hatua.”

Kujiandaa ili kukabilia janga, kwa mujibu wa Guterres kunahitaji uwekezaji mkubwa, akisema kuwa huduma ya afya kwa wote inakuja na gharama lakini bei yake ni rahisi ukilinganisha na hasara ya kutokuwa nayo.

Amesihi kila mtu, nchi na jamii ya kimataifa kuimarisha uwekezaji wa huduma ya afya kwa wote na mifumo thabiti ya afya kuanzia sasa.