Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa wanawake wa kimasai tunatambua haki zetu- Mnufaika Naserian

Maria Mamasita, mmoja wa wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na Naserian. Hapa n wakati aliposhiriki mkutano wa 62 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW62 jijini New York, Marekani mwaka 018.
UN News/Assumpta Massoi
Maria Mamasita, mmoja wa wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na Naserian. Hapa n wakati aliposhiriki mkutano wa 62 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW62 jijini New York, Marekani mwaka 018.

Sasa wanawake wa kimasai tunatambua haki zetu- Mnufaika Naserian

Wanawake

Harakati za Umoja wa Mataifa za kutekeleza lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs la  usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake linaendelea kupigiwa chepuo na wadau mbalimbali likiwemo shirika la kiraia la Naserian wilayan Monduli mkoani Arusha nchini Tanzania.
 

Shirika hilo linalojishughulisha na masuala ya haki na maendeleo ya wajane,  wanawake na wasichana wa jamii ya wamasai limekuwa likiendesha mafunzo ya kubadili mtazamo wa jamii hiyo dhidi ya wanawake na wasichana na miongoni mwa wanufaika ni Maria Mepukori.

Maria wa kijiji cha Mtimmoja kata ya Sejogo anasema “nimepata manufaa ya kuona haki sawa ya mwanamke na mwanaume. Nimepata manufaa kwamba ukielimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima.” 

Mnufaika mwingine kutoka shirika la Naserian ni Grace Mayesiki akisema kujiunga na shirika kumemletea mabadiliko makubwa, “kwa maana wanawake wengi wamebadilika na wamenufaika san  ana elimu inayotolewa ndani ya shirika sana sana upande wa watoto wa kike. Sasa watoto wa kike wa jamii ya kimasai wameona mbele wanasoma. Kwa hiyo jamii imenufaika sana na suala la elimu na pia wanawake wa kijijini wamebadilika, sasa hivi familia zao zinawategemea wao, na wanathubutu kusimama na kujitambua katika familia zao.”

Edward Lenanu ni mjumbe wa shirika la Naserian alipoulizwa ni manufaa yapi ameona kwa wanawake wa kimasai kushiriki katika masuala ya maendeleo, amesema shirika hilo limefungua macho jamii kwa kuwa wanawake waliopata mafunzo wametambua haki zao sawa na wanaume na anaweza kufanya kazi ya kusaidia watoto na kujisaidia mwenyewe mambo yake kama mwanamke na kujitambua zaidi.

Kuhusu maendeleo amesema, “kama tunavyofahamu hakuna maendeleo bila mwanamke na kwa jamii yetu maendeleo mengi yanafanyika na wanawake lakini bila jamii kutambua kuwa wao ndio wenye maendeleo. Kwa sabaau kama mambo ya kuamka na kumuandaa mtoto sawa aende shuleni, mahitaji ya nyumbani ni mwanamke,  na mwanaume yeye kazi yake yeye ambayo ni sisi, mara nyingi ni kuwezesha kidogo hela ya kwenda sokoni, lakini masuala yote ya maendeleo ni mwanamke na siyo mwanaume. “

Wakati harakati zinaendelea kukwamua wanawake wa jamii ya kimasai ili kuleta maendeleo ya jamii, bado kuna wanaume wenye hofu kuwa mila zao zinapotea. Lakini Mepukori Oyeya Mollel anatoa wito kwa wanaume wahamasishe wanawake kujiunga na shirika la Naserian kwa kuwa, “wale waliojiunga wameona mabadiliko na mafanikio makubwa.”

Kwa mujibu wa Mratibu wa Naserian, Alais Esoto, wamekuwa wakipatia mafunzo ya ufugaji bora na mbinu za biashara wanawake wakiwemo wajane ili hatimaye waweze kustawisha maisha yao na familia zao.