Tulichapwa viboko kwa fimbo na nondo,  asema manusura wa kuzama baharini Ghuba

5 Oktoba 2020

Wafanyakazi wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM wamesaidia mamlaka za Djibouti katika kusaka na kuzika mabaki ya wahamiaji wanane waliozama mwishoni mwa wiki na kisha miili yao kusombwa hadi fukweni wakati wakitoka Yemen .
 

Taarifa ya IOM iliiyotolewa leo Obock nchini Djibouti inasema kuwa maiti hao ni miongoni mwa watu 34 wengi wao wakiwa ni wasomali na waethiopia ambao walikuwa wameamua kurejea Afrika baada ya jaribio lao la kusak akazi nchi za kiarabu kuota mbawa. 

“Ilikuwa ni nyakati za usiku na wasafirishaji haramu wa binadamu walizima taa za boti wakidai kuwa tulikuwa tunafuatiliwa na walinzi wa pwani. Lakini walikuwa wanasema uongo,” amenukuliwa Galgalou Haji Wacho kutoka Oroma Ethiopia ambaye ni mmoja wa manusura. 

Amewaeleza maafisa wa IOM kuwa wakati huo hakukuweko na mlinzi yeyote wa pwani “na kisha walianza kutuchapa kwa fimbo na kwa kutumia nondo.”  

Manusura huyo ameongeza kuwa alikuwepo majini kwa takribani saa mbili akihaha kuogelea hadi pwani, akisema “sikuweza kuona chochote, lilikuwa giza totoro, sikufahamu iwapo nilikuwa hai au nimekufa.”

Yeye na wahamiaji wengine 25, ambao baadhi yao walipata majeraha, wanapata matibabu katika kituo cha IOM cha kushughulikia wahamiaji kilichopo Obock nchini Djibouti.

Wakati maelfu ya wahamiaji wa kiafrika wakiwa wamekwama Yemen, mamlaka nchini humo zina hofu kuwa baadhi yao bado wanasubiri fursa nyingine ya kuvuka tena bahari wakati huu ambao baadhi yao walishafanikiwa kufanya hivyo miezi michache iliyopita.Kwa mantiki hiyo kuna hofu ya kuwepo janga lingine katika siku na wiki zijazo.  

Stephanie Daviot, ambaye ni mkuu wa ujumbe wa IOM nchini Djibouti amesema janga la sasa ni wito wa kuwa macho, “wahamiaji wanawasili Djibouti kutoka Yemen kwa kiasi kikubwa. Serikali za ukanda hu una jamii ya kimataifa lazima zishirikiane kushughulikia hali hii ya watu kufanya safari za hatari katikati ya janga la Corona au COVID-19. Wahamiaji ambao hawawezi kuendelea na safari zao na hawana pia uwezo wa kurejea nyumbani.”

Ameongeza kuwa kuhatarisha maisha yao, kukumbwa na ukatili kutoka kwa wasafirishaji haramu na katika mazingira ya sasa wanakumbwa na vifo au majeraha, na shirika lao lina hofu kuwa kunaweza kuwepo na visa zaidi vya wahamiaji kuzama.

Kisa cha mwishoni mwa wiki kinafuatia kuwasili nchini Djibouti kwa wahamiaji 2,678 kutoka Yemen tangu mwezi Julai mwaka huu.
Kutokana na janga la Corona lililosababisha mipaka kufungwa, na njaa kali inayokabili wahamiaji kwenye nchi za ghuba ,wengi wao wamekata tamaa kupata ajira na fursa zozote kwenye ukanda huo.

IOM nchini Djibouti imekuwa ikiwapata wahamiaji hao waliorejea huduma za dharura za matibabu, chakula, maji, mahema na ushauri nasaha kuhusu COVID-19 na kinga dhidi ya ugonjwa huo pindi wanapowasili Obock.

Hata hivyo IOM inaomba msaada zaidi kwa kuzingatia kuwa mwezi Agosti mwaka huu ilizindua ombi la dola milioni 84 kusaidia wahamiaji wa pembe ya Afrika na Yemen, RMRP, ambapo wahamiaji wengi waliokwama Yemen wanataka kurejea nyumbani.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter