Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makazi kwa wote ndio chachu ya mustakbali bora mijini:UN-HABITAT 

Melen, eneo la makazi duni katikati ya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Melen, eneo la makazi duni katikati ya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé

Makazi kwa wote ndio chachu ya mustakbali bora mijini:UN-HABITAT 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuwa makazi bora hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ni suala la uhai na kifo hasa janga la corona likiendelea kusambaa duniani na watu wakitakiwa kusalia majumbani, lakini hatua hiyo haiwezekani hasa kwa wale ambao hawana wanapopaita nyumbani limesema shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT. 

Kaulimbiu ya mwaka huu, “makazi kwa wote, mustakabali bora mijini”  kwa mujibu wa UN-HABITAT, “janga la COVID-19 linatukumbusha kwamba nyumba ni zaidi ya kuwa na paa. Ili kutufanya tujihisi tuko salama na kutuwezesha kuendelea kuishi, kufanyakazi na kusoma, nyumba inahitaji kuwa salama na kuturuhusu kupata huduma za msingi na miundombinu kwa ajili ya hatua za usafi na nafasi ya kutosha kujitenga ili kuepuka maambukizi ya COVID-19.” 

Shirika hilo limeongeza kuwa makazi bora lazima yawe pia katika eneo litakaloruhusu wakazi kufikia maeneo ya umma, fursa za ajira, huduma za afya, shule, vituo vya kulelea watoto na maeneo mingine muhimu ya kijamii. 

UN_HABITAT inakadiria kuwa hata kabla ya janga la COVID-19 watu bilioni 1.8 walikuwa tayari wanaishi katika mitaa ya mabanda na makazi yasiyo rasmi, kwenye nyumba zisizo bora au kutokuwa na makazi kabisa kwenye miji mingi duniani. 

Na zaidi ya hapo, “watu bilioni 3 wanakosa huduma za kunawa mikono na hii inamaanisha mamilioni ya watu kote duniani wana uwezekano wa kuwa na athari za kiafya kutokana na kukosekana kwa huduma za msingi na kuwa kwenye mazingira ya hatari kiuchumi na kijamii.” 

Katibu Mkuu wa UN 

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “dharura ya kuboresha hali ya maisha imeanikwa na janga la COVID-19 ambalo limeathiri maisha ya mamilioni ya watu mijini.  Fursa za upatikanaji wa maji safi na usafi,pamoja na kuweza kujitenga ni muhimu katika kupambana na COVID-19. Hata hivyo katika mitaa ya mabanda imethibitika kuwa ni vigumu kutekeleza hatua hizi. Hii inamaanisha ni ongezeko la hatari ya maambukizi sio tu ndani ya mitaa ya mabanda bali katika miji yote.” 

Ameongeza kuwa pia pengo la kimfumo la usawa limewekwa bayana na janga hili na kuonyesha kwamba watu kutoka jamii za walio wachache, watu wa asili na wahamiaji ndio waathirika wakubwa wa changamoto za makazi, mrundikano na kutokuwa na makazi kabisa. 

COVID-19 imesambaa zaidi katika maeneo ambako watu wanakosa makazi bora na wanakokabiliwa na pengo la usawa na umaskini umesema Umoja wa Mataifa. 

Wakazi katika maeneo hayo mara nyingi pia hawatambuliki na mamlaka au kulindwa na wanakabiliwa na hatari ya kutimuliwa au kuhamishwa kutoka kwenye makazi yao hasa wakati wa majanga. 

Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani ILO asilimia 55 ya watu wote duniani ambao ni karibu watu bilioni 4 hawana faida yoyote wanayopata kutoka aina yoyote ya mifumo ya hifadhi ya jamii. 

Kwa mantiko hiyo shirika la UN-HABITAT linasisitiza kwamba, “makazi au nyumba ni haki ya binadamu na kiini cha haki zingine zote za msingi za binadamu, na ni njia pekee ya kuhakikisha kunakuwepo haki ya miji kwa wote inatimia.” 

Siku ya makazi duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 5.