Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya IFAD imetusaidia wanawake wa Kontagora, Nigeria kuwa mamilionea.  

Mkulima na mpunga baada ya mavuno Bangladesh.FAO yasema bei ya nafaka ilipanda kwa asilimia 4.0 mwezi Agosti.
Picha: IFAD/GMB Akash
Mkulima na mpunga baada ya mavuno Bangladesh.FAO yasema bei ya nafaka ilipanda kwa asilimia 4.0 mwezi Agosti.

Elimu ya IFAD imetusaidia wanawake wa Kontagora, Nigeria kuwa mamilionea.  

Wanawake

Ujuzi uliopatikana kutokana na mafunzo yaliyotolewa kupitia mpango wa msaada wa kifedha kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya chakula na kilimo, IFAD, umewawezesha wanawake katika jimbo la Niger nchini Nigeria kuvuka katika kipindi kigumu cha COVID-19 huku biasahara yao ya mchele ikizidi kushamiri. 

 

Maelfu ya biashara kote duniani zimelazimika kufungwa au zimeshuhudia kuporomoka kwa faida kutokana na janga la COVID-19 lakini kwa wanawake wasindikaji wa mpunga kwenye eneo la Kontagora katika jimbo la Niger nchini Nigeria, si tu wamenusurika lakini pia biashara yao imefanikiwa kifaida hadi asilimia 40.  

Wakati wazalishaji wengine wa mchele walilazimika kusitisha uzalishaji, Asabe Damjuna na wanawake wajasiriamali wenzake wa mchele, walitumia ujuzi wao wa uzalishaji na uuzaji walioupata IFAD, wakaanzisha mfumo wa zamu ambao umewawezesha kuendelea katika mazingira ambayo wengine hawakuweza. Asabe anaeleza,“na tunawezaje kufanya hivyo, lazima tuangalie umbali wa kijamii, kwa hivyo tunafanya kazi kwa zamu wakati wengine wanafanya kazi asubuhi wengine jioni.” 

Asabe na wenzake, kabla ya COVID-19 walikuwa wanauza mchele wao katika shule za eneo hilo, lakini shule zilipofungwa kwasababu ya janga hilo, mlango mmoja unaweza kuwa umefungwa, lakini mwingine ulifunguliwa. 

Kufungwa kwa mipaka ya kimataifa kulimaanisha kuwa soko halifuriki tena na aina nyingine za mchele na hivyo mchele wanaouzalisha wao ukapanda bei kwa asilimia 40. 

Asabe na wanawake wenzake wanaweza kutumia vifaa mbalimbali kwa mujibu wa mafunzo ya IFAD na hii inamaanisha kuwa yeye mwenyewe anaweza sasa kuchakata mchele mara kumi ya ilivyokuwa awali.  

Njia hizi za uchakataji pia zimebadili maisha ya wazalishaji wengine wa mchele kama vile Aishetu, mjane mwenye watoto 12. Mwanamke huyu amekuwa akizalisha mchele kwa miaka 35 bila kupata faida.  

“Kipindi hicho tulikuwa tunauza mchele wetu uliokobolewa katika soko letu la zamani na ilikuwa vigumu kufanya mauzo ya Naira 20,000 kwa wiki bila kujali kazi ngumu tuliyofanya. Kwa hivyo wakati tunapoondoa matumizi, tunabaki bila kitu.” 

Mradi huu umefanikiwa kiasi kwamba wanawake wengi wamekuwa mamilionea katika eneo hilo la Kontagora. Kila mwanamke sasa kwa mwaka anapata kwa wastani wa Naira milioni 6 za Nigeria ambazo ni zaidi ya dola 15,000 za Kimarekani, kiasi ambacho ni zaidi ya anachopata mfanyakazi mkubwa wa umma. Wanawake hao hivi sasa wanamudu kupeleka watoto wao shule, kununua nyumba na magari.