Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu ni wakati muhimu kwa vita dhidi ya COVID-19 kila kiongozi aongeze juhudi:Dkt. Tedros

Kijana anayejitolea akiongoza na kuwafundisha wasichana katika mji katika Yemen, kuhusu njia sahihi ya kunawa mikono.
© UNICEF/Dhia Al-Adimi
Kijana anayejitolea akiongoza na kuwafundisha wasichana katika mji katika Yemen, kuhusu njia sahihi ya kunawa mikono.

Huu ni wakati muhimu kwa vita dhidi ya COVID-19 kila kiongozi aongeze juhudi:Dkt. Tedros

Afya

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Dkt. Adhanom Ghebreyesus leo amemtakia Rais wa Marekani Donald Trump na mkewake Melania Trump ahuweni na kupona haraka baada kupimwa na kugundulikwa kuwa wameambukizwa corona au COVID-19

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi kwa njia ya mtandao Dkt. Tedros amesema, “dunia bado inapitia zahma ya janga la COVID-19. Kila wiki tunaongeza takribani idadi ya wagonjwa milioni 2 na kama mjuavyo dunia imepita idadi ya kihistoria ya vifo milioni 1 wiki hii. Tunawaomboleza watu wengi waliopoteza maisha yao.” 

Mkuu huyo wa WHO ameongeza kwamba, “huu ni wakati muhimu sana katika harakati za kupambana na mlipuko wa corona, tunatoa wito kwa kila kiongozi kuimarisha juhudi za kupambana na janga hili, kuweka mikakati maalum ambayo tunajua itasaidia kuzuia maambukizi zaidi, kuhakikisha kwamba mifumo ya afya na wahudumu wake wanalindwa na kuokoa maisha.” 

Dkt. Tedros amerejea kusema kwamba, “kwetu sote njia ya haraka ya kutusaidia kulishinda janga hili ni kuchukua hatua pamoja.” 

Pia ametangaza kwamba “Tumekamilisha kuidhinisha kipimo cha pili kinachofanyakazi haraka ambacho kitaorodheshwa kwenye vifaa vya matumizi ya dharura. Vipimo hivi ni rahisi kutumia na vinatoa majibu ya kuaminika kwa muda wa takribani dakika 15 hadi 30, badala ya kusubiri masaa au siku kadhaa, na vinapatikana kwa gharama nafuu.” 

Kuna suluhu iko njiani 

Naye Dkt. Mike Ryan wa WHO amesema, “kuna suluhu ambayo huenda iko njiani, kuna ubunifu mkubwa, utengenezaji wa chanjo, tiba na upimaji ambao tunauhitaji. "

Ameendelea kusema kwamba “Kuna kizuizi baina yet una mafanikio hayo n ani kiwango kidogo cha fedha tukifikiria ni kiasi gani ambacho kimekwishatumika na ambacho kimeshatolewa mifukoni kwetu kutoka kwenye uchumi wa dunia. Haya na hususan chanjo havitoi hakikisho la mwisho kabisa lakini ni nyenzo muhimu sana kama zilizvyodhihirisha kufanya kazi siku za nyuma.” 

Kwa mantiki hiyo Dkt.Ryan amesema “Naweza kusema kwamba maneno mazuri ni saw ana tunayahitaji, lakini tunachokihitaji zaidi hivi sasa ni hatua, tunachokihitaji sasa ni uwekezaji na tunachokitaka sasa ni suluhisho.” 

Kwa nini Afrika haijaathirika sana? 

Ameongeza kuwa, “watu wamekuwa wakijiuliza kwa nini Afrika inaonekana kukwepa zahma mbaya na kubwa ya janga hili hadi sasa? Na hilo ni swali zuri, kwa sababu unaweza kujifunza kwa kuuliza swali hilo.” 

Ameelezea kwamba “kwa kiasi ni kutokana na rika kwa sababu nusu ya watu wote Afrika wana umri wa miaka 19 au chini ya hapo na ni asilimia ndogo sana ya watu wana umri wa miaka 65 na zaidi. Na hii inaweza kumaanisha kwamba tuna idadi kuwa ya wagonjwa Afrika lakini vifo ni idadi dogo kutokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya watu wana umri mdogo. 

Lakini pia ameongeza kusema, “ukweli ni kwamba katika baadhi ya nchi za Afrika huenda hakuna upimaji mkubwa unaofanyika, hawana rasilimali na kwa hivyo labda wanabaini wagonjwa wachache na hivyo inadhihirisha wagonjwa wachache na vifo kidogo. Idadi ndogo ya vifo ni sahihi lakini idadi ndogo ya wagonjwa inaweza isiwe sahihi.” 

TAGS: WHO, COVID-19, Afrika, chanjo.