Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika kuadimisha siku ya kupinga machafuko hebu tusitishe uhasama:Guterres 

Njiwa wakiwa wameachiwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani.
UN Photo/Mark Garten)
Njiwa wakiwa wameachiwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani.

Katika kuadimisha siku ya kupinga machafuko hebu tusitishe uhasama:Guterres 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  amerejea wito wake wa kutaka usitishwaji uhasama duniani kote hii leo ikiadhimishwa siku ya kimataifa ya kupinga machafuko ambayo mwaka huu inafanyika kukiwa na athari mbaya za kiuchumi na kijamii zilizotokana na janga la corona au COVID-19. 

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Antonio Guterres amemkumbusha kila mtu kuwa ana wajibu maalum wa kukomesha mapigano na kujikita na adui wa pamoja ambaye ni COVID-19

“Kuna mshindi mmoja tu wa mapigano wakati wa janga la COVID-19 naye ni virusi vyenyewe” amesema Bwana Guterres

Ameongeza kuwa, “wakati janga hili liliposhika kasi nilitoa wito wa kimataifa wa kusitisha uhasama. Leo hii tunahitaji msukumo mpya kutoka jumuiya ya kimataifa ili kufanya wito huu kutimia ifikapo mwisho wa mwaka huu.” 

Usitishwaji uhasama Katibu Mkuu anasema utapunguza madhila kwa kiasi kikubwa, kusaidia kupunguza hatari ya baa la njaa na kuweka mazingira ya majadiliano ya kuelekea amani. 

“Hali ya kutoaminiana imekuwa kikwazo, lakini pia ninaona sababu za kuwa na matumaini. Katika baadhi ya sehemu tunashuhudia usitishaji machafuko” amesema akikumbusha kwamba nchi nyingi wanachama, viongozi wa kidini, mitandao ya asasi za kiraia na wengineo wanaunga mkono wito huo. 

“Sasa ni wakati wa kuongeza juhudi zetu. Hebu tuchagizwe na ari ya Gandhi na misingi ya katiba ya umoja wa Mataifa.” Ameongeza Katibu Mkuu. 

Nguvu ya kutokuwa na machafuko na maandamano ya amani 

Katika ujumbe huo Katibu Mkuu pia amesema siku hii ya kimataifa inaainisha nguvu kubwa ya kutokuwa na machafuko na maandamano ya amani. 

“Ni kumbusho muafaka la kuenzi na kukumbatia maadili aliyoishi Gandhi ya kuchagiza utu, ulinzi sawa kwa wote na kwa jamii kuishi pamoja kwa amani.” Amesema. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio mwaka 2007 liliitenga tarehe 2 Oktoba kuwa siku ya kimataifa ya kupinga machafuko ili iende sanjari na siku ya kuzaliwa na Mahatma Gandhi ambaye aliongoza vuguvugu la India kupata uhuru na kuchagiza dhana ya mkakati wa kupinga machafuko.