Wahamiaji wakumbwa na mateso yasiyo ya kawaida baharini Mediteranea 

2 Oktoba 2020

Mateso wanayopitia wahamiaji wanaojaribu kuvuka bahari ya Mediteranea ili kusaka hali bora Ulaya ni ya kutisha, imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, hii leo. 

Taarifa ya ofisi hiyo iliyotolewa Geneva, Uswisi,  imesema timu yake iliyokwenda kufuatilia hali za wahamiaji wanaopitia Libya kabla ya kuvuka baharí, imebaini ghasia ambapo watu ambao tayari walikumbwa na machungu Libya, wameachwa baharini kwa muda mrefu, wengine boti zao kuingiliwa kwa vurugu na hatimaye kuswekwa korokoroni, kuteswa na haki zao kukiukwa. 

“Kwa wale ambao waliokolewa na hatimaye kufika katika fukwe za Ulaya, nao pia huwekwa korokoroni kinyume cha  sheria, katika mazingira dhalili huku wakiteswa. Hali imekuwa mbaya zaidi wakati huu wa janga la Corona au COVID-19 ambapo boti za uokozi na zile za kutoa huduma za kibinadamu zimezuiwa kuendelea na kazi yao ya kuokoa maisha,” imesema taarifa ya OHCHR ikiongeza kuwa hata mashirika ya kibinadamu yanazuiwa kwenda kutembelea wahamiaji na kuwapatia misaada. 

Timu hiyo iliyokwenda kusaka ukweli ilifika hadi Malta na kuwepo nchini humo tangu tarehe 21 hadi 26 mwezi uliopita wa Septemba ambako walizungumza na maafisa wa serikali, wadau wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa wahamiaji, mashirika ya kiraia na wahamiaji 76. 

Miongoni mwa wahamiaji hao, 41 ni wanaume, 22 ni wanawake, 13 ni watoto na wote wanatoka mataifa 25. 

Wakifafanua mateso waliyopitia baharini, wahamiaji hao wamesema kuna wakati, “boti zinashambuliwa kwa risasi na kikosi cha walinzi wa pwani cha Libya na kusababisha boti kuzama au watu kulazimika kujirusha baharini ili kujiokoa.” 

Kuna ripoti ya kwamba katika tukio moja wanajeshi wa Malta walijaribu kusukuma boti ili irejee Libya. 

Ni kwa mantiki hiyo ofisi hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inatoa wito wa dharura wa kushughulikia hali mbayá inayokumba wahamiaji wanaosaka kuingia Ulaya kupitia baharí ya Mediteranea. 

Akizungumzia changamoto zinazoendelea dhidi ya wahamiaji, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema, “shinikizo katika vituo vya mapokezi Malta vimekuwa vinatambulika lakini janga la Corona limefanya hali kuwa mbaya zaidi. Serikali zinakabiliwa na changamoto kutokana na COVID-19, lakini licha ya changamoto hizo, haki za binadamu lazima kwanza zizingatiwe na wale walioko korokoroni nao wasisahauliwe.” 

OHCHR inasema licha ya hatari na machungu, bado wahamiaji wanaendelea kufanya safari hiyo hatari, hata wengine kujaribu tena na tena kutokana na ukosefu wa njia salama za uhamiaji. 

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud